Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel amesema ipo haja ya Serikali kupitia Taasisi ya RUWASA kuangalia upya namna ya kuwa na chombo kimoja cha Watumia Maji ili kuondokana na changamoto za usimamizi zinazoikabili sekta ya maji vijijini.
Aidha kupitia Hotuba yake alionya vikali matumizi ya fedha mbichi (zisizowekwa benki) jambo ambalo limekuwa likijitokeza kwenye baadhi ya vyombo vya watumia maji (CBWSO).
Mhe. Mwema alisema hayo wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa wadau wa sekta ya maji wa nusu mwaka ulioratibiwa na Wakala wa maji na usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Kongwa Novemba 3, 2023 kuhusu hali ya upatikananji wa maji safi na salama Wilayani Kongwa na programu ya Lipa kwa Matokeo P4R.
Akiunga mkono Rai ya Mkuu wa Wilaya, Kaimu Meneja wa RUWASA Mkoa wa Dodoma Mhandisi Bazil Mwiserya alisema RUWASA inaendelea na jitihada za makusudi za kupunguza utitiri wa vyombo vya watumia maji ili kuboresha utoaji wa huduma bora za maji na kwamba ni Matamanio yake kuona Rai ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa inatekelezeka na hivyo kuifanya Kongwa iwe fursa ya wengine kujifunza.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri, Makamu Mwenyekiti Mhe. Richard Mwite na Diwani wa kata ya Mkoka alisema Licha ya changamoto ya Upungufu wa huduma ya maji katika baadhi ya maeneo, Halmashauri imekuwa ikipata ushirikiano wa kutosha kutoka RUWASA tangu Taasisi hiyo ilipojitegemea chini ya Wizara maji na kwa kipindi chote wamekuwa wakiwasilisha taarifa kwenye vikao vya Baraza la Madiwani mara kadhaa kwa lengo la kupokea ushauri.
Akiwasilisha taarifa katika Mkutano huo wa wadau, Meneja Ruwasa Wilaya ya Kongwa Mhandisi Nyamwanja Bwire alibainisha changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma jitihada za Taasisi hiyo ikiwemo ukiukwaji wa makusudi wa miongozo na taratibu za uendeshaji wa huduma za maji vijijini, mwingiliano baina ya serikali za vijiji na vyombo vya watumia maji na uwepo wa maji chumvi chini ya ardhi hali inayoathiri upatikanaji wa maji ya kutosha.
Akitoa Mafunzo katika Mkutano huo Afisa Maendeleo ya Jamii RUWASA Mkoa wa Dodoma Bi. Prisilla Mkilanya alisema Kwa mujibu wa maelekezo ya Mkurugenzi mkuu wa RUWASA, kufikia Mwezi DIsemba, 2023 vyombo vya watumia maji mkoani Dodoma vinatakiwa kupunguzwa hadi kufikia walau 15 kwa kila Wilaya.
Kuhusu wazo la kuwa na chombo kimoja cha watumia maji, Bi. Mkilanya amesisitiza kuwa mchakato huo huenda ukachukua muda mrefu hivyo wakati ukiendelea wa wadau watambue kuwa ni vema kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya maji na Usafi wa Mazingira namba 5 ya mwaka 2019, mada iliyofafanuliwa na Mwanasheria wa Halmashauri. Bwana Lenatus Pauline.
Akiwasisilisha mada katika Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kongwa Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri Bwana Jacob Lutana Mugusi alithibitisha kuwepo kwa changamoto ya matumizi ya fedha mbichi katika Kata za Mlali na Mtanana ambapo zaidi ya shilingi Mil. 22 hazikuwa na nyaraka halali za matumizi.
Kufuatia hoja ya Mkaguzi wa ndani, Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Kongwa ikiwakilishwa na Bwana Hamad Kibwana imetoa elimu ya Rushwa na athari zake kwa wadau wa maji, na kwamba Taasisi hiyo haipo tayari kufumbia macho vitendo vya Rushwa, ikiwa ni Pamoja na Matumizi ya Fedha mbichi.
Akiwakilisha chama cha Mapinduzi (CCM) Mwenyekiti wa chama Mwl. Abdi Mussa Matari alisema Ni vema Ruwasa kupitia vyombo vya watumia maji ikajitegemea kwa kukusanya mapato kikamilifu badala ya kuitegemea Serikali.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.