Wananchi wa Wilaya ya Kongwa wameaswa kumshukuru kwa dhati rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha mikopo ya asilimia kumi ambayo ilisimama kutolewa kwa muda.
Hayo yameongewa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Mayeka Simon Mayeka ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni mia mbili na sabini na saba kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Pia DC. Mayeka amewaeleza wanawake waliohudhuria katika hafla hiyo kuhusu bahati waliyonayo sababu anayeongoza nchi ni mwanamke kama wao na anafahamu changamoto zao kiundani bila hata kuambiwa, hivyo waitumie faida hiyo kuchangamkia fursa mbalimbali ambazo Mhe. Rais anawapatia ili kuunga mkono juhudi zake na kundi kubwa la wanawake kujikwamua kiuchumi.
DC. Mayeka ametengua uvumi ambao umekuwa ukisikika kuhusu fedha za mikopo ya asilimia kumi ambao baadhi ya wananchi wamekuwa wakisambaza kuwa fedha hizo hata vikundi visiporejesha havitadaiwa na katika mwaka wa uchaguzi hakuna kikundi kitakachodaiwa kwa kusema hu oni uongo na waelewe kuwa Uchaguzi ni jambo linguine na lenye umuhimu katika Taifa lakini mkopo ni swala linguine ambalo halihusiani na Uchaguzi hivyo wasidanganyane sababu marejesho ya fedha hizo yatapelekea na vikundi vingine kunufaika kwa wao pia kupata fedha hizo.
DC. Mayeka ameeleza kuwa ni nia njema ya Serikali kuona mikopo hiyo inatafsiriwa kwa mabadiliko ya maisha yanayoonekana waziwazi katika jamii. DC. Mayeka pia amepongeza baadhi ya vikundi ambavyo vilikopa na kurejesha kwa uaminifu na kuomba mikopo kwa awamu nyingine na kutoa rai kwa vikundi vingine kuiga mfano wa vikundi hivyo.
Akisoma taarifa fupi ya mikopo ya asilimia kumi ya Halmashauri, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii ameeleza kuwa kama ilivyo ada Halmashauri ilichakata maombi ya vikundi yanayotumwa katika mfumo wa wezesha ambapo maombi 87 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.6 yalitumwa kwenye mfumo na baada ya kamati kuchakata kwa kutumia kanuni za utoaji mikopo, kamati ilipendekeza na kuidhinisha mikopo kwa vikundi 21 ambapo fedha zimeshawekwa kwenye akaunti za vikundi husika.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kongwa Bi. Sozi Ngate ameeleza kuwa lengo la serikali ni kuwezesha na kusaidia wananchi kujikimu kimapato kwa kuwapatia mitaji inayopatikana katika mikopo hiyo. Na ameeleza kuwa kamati inahusisha vyombo mbalimbali ikiwemo vyombo vya usalama ili kuhakikisha haki inapatikana katika ugawaji mikopo pamoja na kusaidia katika urejeshwaji wa mikopo hiyo. Pia amewapongeza wanavikundi waliofanikiwa kupata mikopo na kuwakumbusha kufata kanuni na sheria pamoja na miongozo ambayo ipo katika mikataba yao waliotia Saini.
Akiongea kwa wakati wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa dkt. Omary Nkullo licha ya kuwapongeza wanavikundi waliopata mikopo hiyo isiyokuwa na riba, lakini pia amewakumbusha kuwa mikopo waliyopata sio zawadi bali ni mikopo inayotolewa kutokana na agizo la Serikali kuwa fedha zinazotokana na kodi za wananchi asilimia kumi itolewe ili kukopesha makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na inatakiwa irejeshwe ili na vikundi vingine vinufaike na mikopo hiyo ili kusudi mikopo hiyo iwafikie watu wengi zaidi.
Akizungumza baada ya kupokea mkopo, Bi. Debora Boma ambaye ni mwanakikundi wa kikundi cha Nyemo Group kinachojishughulisha na ufugaji wa Samaki kinachopatikana Kata ya Kibaigwa, ameeleza furaha ya kikundi kupata mkopo na kutoa shukrani zake za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kurejesha mikopo hiyo na kuahidi kuwa mkopo huo utafanya kazi iliyokusudiwa na fedha walizokopa zitarejeshwa kwa wakati kama jinsi ambavyo mkataba wa mkopo unavyoelekeza.
Naye Mohamed Said, Mwenyekiti wa kikundi cha Mshikamano Mtanana Group kinachojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji ametoa shukrani zake za dhati kwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na uongozi wa Halmashari ya Wilaya ya Kongwa kwa mchakato mzima uliojikita katika haki ambao umepelekea vikundi vyenye sifa kupata mikopo hiyo, Bw. Said ameeleza kuwa ni dhima ya kikundi kubadili taswira ya kuwa kilimo ni cha wazee na watu wanaostaafu kwa kufanikiwa katika sekta hiyo kama vijana ili kuwa mfano kwa vijana wengine kujikita katika shughuli hiyo na kuacha kulalamika kuwa hakuna ajira.
Hii ni awamu ya pili ya utoaji wa mikopo ya asilimia kumi ambayo kwa awamu ya kwanza vikundi hamsini na nne vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilikabidhiwa shilingi milioni mia tano sitini na tano ambapo katika awamu ya pili, vikundi ishirini na moja vimekabidhiwa shilingi milioni mia mbili sabini na saba laki tatu tisini nan ne n amia nne themanini nan ne kama inavyoelekezwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuwa Halmashauri zitoe asilimia kumi ya mapato yake ili kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa dhumuni la kuinua maisha ya wananchi na kuwaongezea kipato.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.