Vikundi Wilayani Kongwa vimekabidhiwa hundi ya shilingi milioni mia tano na sitini na tano katika awamu ya kwanza ya ugawaji mikopo. Mikopo hiyo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu Inaelekezwa na chama cha Mapinduzi kupitia ilani yake kuhakikisha Maisha ya wananchi yanainuliwa kupitia kupelekwa kwa mikopo ya asilimia kumi kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Vikundi Hamsini na nne vimepatiwa mkopo kwa awamu ya kwanza ambapo uteuzi umefanyika vizuri hadi kupelekea vikundi hivyo kuchaguliwa ili kunufaika na mikopo hiyo.
Mgeni rasmi pamoja na viongozi wengine wa Serikali wakikabidhi hundi yenye thamani ya mikopo iliyokabidhiwa wa vikundi.
Akiongea wakati wa kukabidhi mikopo hiyo, mgeni rasmi mhe. Mayeka S. Mayeka, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa ameeleza kuwa nia ya mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuinua hali ya kiuchumi ya wananchi ni njema kwani milioni mia tano ingeweza kujenga vituo vya afya, madarasa, na miundombinu mingine lakini imeenda kutolewa kwenye vikundi ili wananchi wainuliwe hali yao ya kiuchumi.
Mgeni rasmi Mhe. Mayeka S. Mayeka akihotubia wanavikundi wakati wakisubiria kupatiwa mikopo.
Mhe. Mayeka amewasifu wenye vikundi vinavyofanya vizuri katika kurudisha mikopo na kutolea mfano vikundi ambavyo vilishakopa na kurudisha mikopo kwa uaminifu hivyo kupelekea kupata mkopo kwa awamu nyingine mwaka huu.
Moja ya vikundi hivyo ni kikundi cha bodaboda ambacho DC. Mayeka ameeleza kuwa kimefanya vizuri huko nyuma katika marejesho hivyo kufanya kupata mkopo kwa awamu nyingine na ameonyesha matamanio yake kuona kikundi hicho kikifikiria mbali zaidi ya bodaboda na kuendelea zaidi kwenye sekta hiyo ya usafirishaji.
Aidha Mhe. Mayeka ametoa rai kwa wanavikundi kuhusu marejesho ya mikopo ambayo bado baadhi ya vikundi havijarudisha na amewaasa kuondoa mtazamo uliokuwa mwanzoni kuwa fedha ya serikali ni ya kutumia pasi kurudisha. Pia Mkuu wa Wilaya ameelezea tatizo la migogoro kwa vikundi pale ambapo wanapata pesa hizi za mikopo na kueleza kuwa mafanikio hayawezionekana kwa njia hiyo ya migogoro mara pale ambapo vikundi vinawekewa pesa hizo kwani hii hupelekea vikundi kuvunjika na kuingia katika madeni.
DC. Mayeka amemaliza kwa kushauri wanavinkundi wafanye vizuri katika miradi yao kwa kutumia vizuri pesa walizopewa ili waweze kurejesha mikopo hiyo na kufanya Wilaya ya Kongwa kuwa Wilaya ya mfano katika ufanisi wa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, pia amewaasa vijana wenye fani wakimbilie fursa hizi za mikopo na wasiendelee kulalamika kuwa hakuna ajira na hakuna mitaji kwani serikali inatoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya mikopo ili kuwezesha wananchi wake wajikwamue kiuchumi.
Kwa upande wake Mbunge na spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai akiongea na wanavikundi amerejelea msemo wa, “Kama umezaliwa maskini, huna wa kumlaumu, ila ukifa maskini wakulaumiwa ni wewe mwenyewe.” Wakati akisisitiza kuwa mikopo hii ni fursa mahsusi kwa wananchi kujikwamua kutoka kwenye janga la umaskini na kuinua Maisha yao kiuchumi. Pia ameongeza kuwa matajiri wengi wametumia mikopo kuongeza utajiri wao hivyo hata wanavikundi wakitumia mikopo hii kwa uaminifu kutekeleza mipango waliojiwekea basi ni dhahiri kuwa watanufaika nayo.
Dirisha la utoaji mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu lilifunguliwa rasmi tarehe 1 Oktoba mwaka huu kwa ajili ya vikundi kuomba fursa ya mikopo hiyo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.