Timu ya wataalam kutoka Idara ya maendeleo ya jamii imefanya ziara ya ufuatiliaji na tathmini kwa vikundi 47 vya Kata 16 vilivyonufaika na mkopo awamu ya kwanza Wilayani Kongwa kwa lengo la kuhakiki Miradi ya vikundi hivyo ili kujionea mwenendo wa miradi hiyo, changamoto na mafanikio ili kuwashauri waweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Bwana Alphonce Mkwizu Afisa Maendeleo ya Jamii ameeleza kuwa tathmini na ufuatiliaji wa fedha hizo za 10% ya Halmashauri kwa wanawake vijana na watu wenye ulemavu imeonesha kuwa kuna changamoto nyingi katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanywa na vikundi zikiwemo shughuli za Kilimo cha umwagiliaji wa mazao ya biashara, maduka ya Dawa, maduka ya nguo, viwanda vidogo vidogo, maduka ya chakula, ufugaji, usafirishaji nk.
Aidha Ndg Mkwizu amesema kuwa changamoto zilizobainika ni pamoja na vikundi kubadili matumizi ya fedha ya mkopo bila kutoa taarifa kwa mtendaji na menejimenti akitolea mfano baadhi ya vikundi vilivyoomba fedha kwaajili ya kununua pikipiki lakini vikaenda kufanya biashara ya kununua na kuuza mazao.
Aidha Ndg Mkwizu ameongeza kuwa changamoto nyingine ni vikundi kushindwa kuweka akiba, kuwepo kwa migogogoro baina ya wanavikundi na kufanya kazi kwa mazoea bila kushirikisha wataalam kama vile maafisa ugani,maafisa biashara na viongozi wao wa Vijiji ili kuwasaidia kutatua changamoto wanazokutana nazo na kuwasaidia kupata matokeo bora zaidi ya kuwawezesha kupata marejesho.
Ndg. Joseph Mshana Afisa maendeleo ya jamii katika kutatua changamoto hizo amesisitiza wanavikundi kujisimamia katika kuweka akiba kwa kutekeleza agizo la kimwongozo ili kujiandaa na kujenga msingi mzuri wa marejesho unaotarajia kuanza Mei 8 na kuwakumbusha wafanye kazi kama walivyopanga katika katiba zao za vikundi na watumie fursa hiyo inayotolewa na Serikali kuhakikisha wanajikwamua na hali za maisha walizonazo.
Pia Ndg Mshana amewataka wanavikundi kushirikisha viongozi kwa kila hatua ya utekelezaji wa shughuli zao, kuweka kumbukumbu ya risiti ya kila kifaa wanachonunua ili kujenga uaminifu na kusisitiza kutumia vizuri fursa hiyo ya fedha za mkopo walizopata kwani watu wengi wanatamani kupata fursa ambazo wamezipata.
Mkuu wa Divisheni ya maendeleo ya jamii Wilaya ya Kongwa Bi. Paskalina Duwe ameagiza maafisa maendeleo ya jamii Kata kufuatilia vikundi kuhakikisha vinatekeleza maagizo yote yanayotolewa katika vikao pamoja na kutatua changamoto zinazokabili vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kurejesha mikopo.
Kwa upande wao baadhi ya wanavikundi wametaja changamoto wanazokutana nazo kuwa ni mifugo kuugua hadi kufa, pamoja na mabadiliko ya bei ya kununulia mifugo hali inayopelekea kuwa na idadi ndogo ya mifugo au kununua mifugo ambayo haina ubora.
Bi Elizabeth Chidabile kutoka kikundi cha Mtazamo Chanya kilichopo kijiji cha Makawa kinachojishughulisha na Kilimo cha umwagiliaji mbogamboga na matunda kilichopatiwa mkopo wa shilingi milioni 21.4 anasema kuwa awali walilima kienyeji hawakupata mazao bora lakini baada ya Afisa ugani kuwapa elimu wameanza kulima kitaalam zaidi na mazao yameongezeka.
Pamoja na hayo wanavikundi hao wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia mikopo hiyo ambayo imesaidia kuwa na mitaji ya kufanya biashara na kujikwamua kiuchumi kwa kujiajiri, kuwa na makazi bora, kusomesha watoto, kukidhi mahitaji mengine ya familia na kutoa ajira kwa wanajamii.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.