Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa imepongezwa kwa kupata hati safi kwa mwaka wa Fedha ulioishia Juni, 2022.
Pongezi hizo zimetolewa na Viongozi mbalimbali katika Mkutano wa baraza la Madiwani uliofanyika tarehe 27 Julai, 2023 kupokea na kujadili taarifa za robo ya nne ya Mwaka wa Fedha 2022/2023, nyingi zikielekezwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Dkt. Omary Nkullo na Wakuu wa Divisheni na Vitengo.
Akihutubia baraza hilo, Mkuu wa Wilaya Mhe. Remidius Mwema Emmanuel amesema kitendo Cha Halmashauri kupata hati safi ni Zawadi kubwa Kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe Mwema alitoa wito kwa Madiwani kuwa walezi wa wataalamu waliopo katika Maeneo yao wakiwemo Walimu ili kwa pamoja waweze kutokomeza utoro Shuleni kwani pasipo kufanya hivyo hakuna sababu ya kuboresha miundombinu ya shule.
Akizungumza katika hotuba ya Ufunguzi, Mwenyekiti wa baraza hilo Mhe. White Zuberi Mwanzalila alisema Halmashauri hiyo imepata hati safi baada ya ukaguzi wa mdhibiti na mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) jambo alilolitaja kuwa si lelemama.
Aidha katika taarifa ya Mwenyekiti iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji (W) Dkt. Omary A. Nkullo, Katika kipindi hicho Halmashauri iliidhinishiwa kutumia jumla ya shilingi......ambapo iliweza kukusanya asilimia 95% ya mpango wa bajeti.
Kufuatia taarifa hiyo, Kaimu Katibu wa chama cha Mapinduzi (CCM) Bwana Emmanuel Msemwa ameipongeza Halmashauri na kuitaja miongoni mwa Halmashauri zisizo na Migogoro.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa DodomaAfisa Utumishi ofisi ya Mkoa wa Dodoma Bi. Prisca Lusoli alisema Mkuu wa Mkoa Mhe. Rosemary Senyamule anatoa pongezi kwa Halmashauri kwa kukusanya Mapato kwa asilimia 95% kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Juni, 2023 na kutoa Rai Kwa Halmashauri kuongeza jitihada katika ukusanyaji wa Mapato ya ndani na kuhakikisha inazingatia taratibu za matumizi ya fedha ili kuepuka hoja za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG)
Akitoa maoni yake Bi. Prisca aliwaasa Madiwani kujenga utamaduni wa kuwasiliana na Taasisi mbalimbali zinazotoa huduma Kwa wananchi badala ya kusubiri vikao.
Katika baraza hilo Taasisi mbalimbali ziliwasilisha taarifa za Utekelezaji wa miradi mbalimbali sambamba na kujibu changamoto mbalimbali.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.