Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Katibu Tawala Wilaya ya Kongwa Bi. Sozi Ngate amewataka viongozi wa Serikali za Kata na vijiji kuitisha mikutano ya kisheria ili kuwapa taarifa mbalimbali wanananchi, ikiwemo mapato na matumizi.
Bi. Ngate amesema hayo wakati akihutubia Wananchi wa Kata ya Chitego akiwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Familia duniani yaliyofanyika Kijiji cha Chitego kwa ngazi ya Wilaya Mei 15, 2024.
Wa pili kushoto ni Katibu Tawala (W) Bi. Sozi Ngate akishiriki Maadhimisho kama mgeni rasmi.
Akijibu miongoni mwa kero za Wananchi kuhusu migogoro ya ardhi, Bi. Ngate alisema ni lazima uchunguzi ufanyike kuhusu tuhuma za kukodishwa shamba la kijiji na fedha kutumiwa nje ya taratibu, huku akiwataka Wananchi kuwa mstari wa mbele kushiriki mikutano na vikao vinavyoitishwa na viongozi wa vijiji na Kata " Suala la shamba la Kijiji tutaleta mkaguzi wa ndani ajiridhishe: Na kama kuna ubadhirifu tutachukua hatua, hakuna aliye juu ya Sheria". Alisema Ngate.
Sanjari na hayo amewataka Wananchi kuzingatia malezi bora kwa watoto wao, ikiwa ni pamoja na kuchangia chakula ili watoto wao waweze kusoma kwa furaha, huku akikemea Suala la utoro shuleni.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu Bi. Paskalina Duwe alisema kupitia picha kutoka kwa watoto, hali ya malezi kwa watoto kwa Sasa ni changamoto, hivyo ni lazima tofauti kati ya wazazi ziwekwe pembeni ili kuepuka kuathiri maendeleo ya watoto kwa kudumisha amani na upendo wa familia.
Bi. Paskalina Duwe Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Kongwa
Naye Diwani wa Kata ya Chitego Mhe. Peter Y. Kalunju alitoa pongezi kwa Serikali kwa kutekeleza miradi mbalimbali katika Kata hiyo ikiwemo mradi wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 147 uliopo kitongoji cha Mgoroka, Kijiji cha Ngutoto ingawa ameiomba Serikali kutatua changamoto ya barabara inayounganisha Kijiji cha Leganga na Chitego kwani kwa Sasa Wananchi wanatumia gharama kubwa kuzungukia Kata ya Zoissa wakati ipo barabara hiyo ya mkato.
Diwani wa Kata ya Chitego Mhe. Peter Kalunju akiwasilisha kero ya Barabara mbele ya meza kuu na Wananchi.
Akizungumzia mikakati ya mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, Afisa wa polisi anayeshughulikia dawati la Jinsia, D/SGT Zaibabu Zuberi Halfan alisema lazima familia ziache malumbano ili kujenga familia bora.
D/SGT Zainabu Zuberi Halfan - Mkuu wa Dawati la Jinsia Polisi Kongwa akizungumza na Wananchi.
Akizungumza na Wananchi Afisa Tarafa wa Tarafa ya Zoissa Bwana Denis Mbawi Semindu aliwataka Wananchi wa Kata hiyo kutoa ushirikiano wa Kutosha kwenye Zoezi la Mafunzo ya Jeshi la Akiba yanayotarajia kufanyika katika Kata hiyo.
Katika Maadhimisho hayo, Wananchi wamewasilisha kero mbalimbali ambazo viongozi wameahidi kuzishughulikia kikamilifu.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.