Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Viongozi wa kisiasa wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea maslahi ya watumishi wa umma waliopo kwenye maeneo yao ili kuchochea kasi ya Maendeleo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhe. White Zuberi Mwanzalila, wakati akizungumza na wadau wa Elimu katika kikao cha mwaka cha wadau , Jumamosi ya Tarehe 11 Machi 2023 katika ukumbi wa shule ya Sekondari Kongwa.
Mhe. Mwanzalila alisema, Watumishi wa umma waliopo katika maeneo mbalimbali ya kiutawala, wapo kwa ajili ya kusaidia jamii katika nyanja mbalimbali za maendeleo na siyo maadui kwa viongozi wa kuchaguliwa.
’’Hawa Watumishi ambao wameletwa kwenye maeneo yetu, wamekuja kutusaidia kuwaendeleza wananchi wetu na sisi wenyewe, hawa siyo maadui zetu.’’ Alisema Mwanzalila.
Kuhusu wazazi wasiojiweza kiuchumi, Mhe. Mwanzalila alisema; Halmashauri itawanunulia mahitaji yote ya msingi wanafunzi watakaofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na kwa wanafunzi watakaofaulu kwa daraja la kwanza na kukosa nafasi kwenye shule za bweni, Halmashauri imetenga bajeti kuziwezesha shule mbili za bweni za Zoissa na Sejeli kuwapokea kama motisha kwa kufanya vizuri mitihani yao.
‘’ Tunazo shule mbili za sekondari ambazo zina mabweni tayari, Tumemwelekeza mkurugenzi; Hawa Watoto ambao wamepata daraja la kwanza tunataka tuwakusanye kama Mkoka itakuwa shule ya wasichana itakuwa ya wasichana tupu’’ Mwanzalila.
Akiwasilisha taarifa ya tathmini ya hali ya ufaulu kwa shule za msingi na sekondari, Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Kongwa Bi. Margareth Temu alitaja changamoto zinazorudisha nyuma ufaulu wa wanafunzi kuwa ni pamoja na upungufu wa walimu, ukosefu wa chakula shuleni, mwamko duni wa jamii, utoro, mmomonyoko wa maadili na miundombinu ya madarasa.
Ili kupunguza changamoto hizo Bi Temu amesema Jamii inapaswa kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao ikiwemo walimu wastaafu na wasio na ajira.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya Huduma za Jamii na Diwani wa Kata ya Sejeli Mhe. Chilingo Chimeledya alikemea tabia ya wazazi kushawishi Watoto wao kukataa masomo, na ameahidi kuwa yeyote atakayebainika tashughulikiwa.
Aidha Mhe. Chimedya amewaasa watumishi kudumisha upendo baina yao, na kuwataka viongozi wa vijiji na kata kuwatembelea ili kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili.’’Kuna baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji hawatembelei shule, yaani wao wanajua shule ni kitu kingine na wao ni kitu kingine. Tukifanya hivyo hatutafanikiwa’’ Mhe. Chimeledya.
Katika kikao hicho walimu na wadau wengine wa elimu walichangia mada mbalimbali zikiwemo mbinu za kuboresha ufundishaji shuleni pamoja na kutoa mapendekezo yao. Kufuatia hatua hiyo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nhembo Bwn. Jeneck Mpinge, ameiomba Wizara ya Elimu kufuta Mambo yote yasiyo ya lazima yanayopunguza muda wa mwalimu kufundisha kwani shule yake imefanikiwa kufanya vizuri baada ya kuweka kipaumbele kwenye ufundishaji. ‘’Tumepunguza kidogo uumini wa maandishi maandishi, tunachokifanya sisi Nhembo mwalimu akifika breki ya kwanza nenda kafanye kazi’’ Mwl. Mpinge .
Akizungumza kuelekea hitimisho la kikao, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo alisema Jamii inapaswa kushiriki kikamilifu kwenye kutatua changamoto zinazoikabili ikiwemo masuala ya Elimu licha ya uwepo wa Nguvu ya serikali.
Akihitimisha kikao hicho, Mgeni Rasmi Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa amewataka viongozi kusimamia kikamilifu miradi yote inayoendelea na pale inapotokea changamoto watoe taarifa kwa ajili ya ufuatiliaji.
Katika Hafla hiyo Mgeni Rasmi alikabidhi zawadi mbalimbali zilizoandaliwa na Halmashauri kwa wanafunzi, walimu na shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya taifa kwa mwaka 2022
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.