Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Wazazi Wilayani Kongwa wametakiwa kufanya jitihada za makusudi kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni.
Rai hiyo imetolewa na kamati ya lishe Wilaya ya Kongwa wakati wa kikao chake cha kawaida kilichoketi Januari 22, 2024 katika ukumbi wa Hospitali ya Wilaya kikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Bwana Fortunatus Mabula.
Wakichangia hoja mbalimbali wajumbe wa kikao hicho kwa pamoja wameshauri ushirikiano uimarishwe baina ya walimu, wazazi na viongozi wa serikali za kata na vijiji ili kufanikisha michango ya chakula shuleni.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Shughuli za lishe, Afisa Lishe Wilaya ya Kongwa Bi. Maria Haule alisema hali ya upatikanaji wa chakula shuleni imepanda kutoka 25% mwaka jana hadi kufikia 75% mwaka huu baada ya jitihada za idara za halmashauri kutenga bajeti ya kununua chakula na kukipeleka shuleni.
Kwa upande wao wadau wa Lishe Wilayani Kongwa, wameeleza jitihada walizochukua kuboreha lishe ambapo Bi. Flora Manyanda wa CUAMM alisema kwa Sasa Wilaya ya Kongwa haina upungufu wa chakula dawa kwa watoto katika vituo vyote vya kutolea huduma, huku akisisitiza wananchi kushiriki katika mikutano ya siku ya Afya na Lishe katika maeneo yao.
Naye Bwana Simon Kutamika, Afisa Miradi World Vision Wilaya ya Kongwa alisema Shirika lake limetumia zaidi ya shilingi milioni saba kufanya tathmini ya hali ya lishe katika kata tatu zenye jumla ya vijiji 10 na itakuja na matokeo hivi karibuni.
Akitilia mkazo taarifa yake, Afisa Elimu ya Awali na Msingi Wilaya Mwl. Margareth Temu alisema ili shule ziweze kuzalisha chakula ni vizuri Serikali za vijiji zitenge maeneo ya mashamba ya shule, kwa kuwa shule nyingi hazina fedha za kukodi mashamba.
Kati ya wanafunzi 103,984 jumla ya wanafunzi 76,973 ndio wanaopata chakula shuleni sawa na 74%
Mwl.Temu aliongeza kuwa Ili huduma ya upatikanaji chakula shuleni iwe endelevu, jamii inapaswa kutambua umuhimu wa kuchangia, sambamba na kujenga uaminifu kwa walimu, ili waweze kuchagia kiasi cha kuwezesha wanafunzi kupata chakula kwa kipindi kirefu.
Itakumbukwa kuwa, katika ziara ya kwanza ya Mhe. Mayeka Simon Mayeka Kata ya Mkoka, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa alinukuliwa akisema "Siri ya Ufaulu wa wanafunzi ni kupata chakula shuleni" Mhe. Mayeka alisema.
Hivyo Wazazi wameshauriwa kujenga Imani kwa walimu na kuachana na dhana potofu kuwa walimu wanaweza kupunguza chakula kinachochangwa Kwa ajili ya Wanafunzi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.