Tatizo la utoro shuleni limetajwa kuwa sehemu ya vikwazo kwa jitihada za walimu za kuwapatia stadi na maarifa wanafunzi katika maeneo mbalimbali Nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Enock Msonde, wakati wa ziara yake Wilayani Kongwa Jumamosi ya Mwisho ya Mwaka 2022.
Kupitia kikao hicho Maalum katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Dkt. Msonde aliwashauri viongozi kushirikiana na walimu katika kubuni na kutekeleza mikakati ya kudhibiti utoro ikiwa ni pamoja na kulifanya tatizo hilo kuwa miongoni mwa agenda za kudumu katika vikao mbalimbali.
Katika hatua nyingine Dkt. Msonde ametembelea na kukagua ujenzi wa shule mpya mbili za sekondari za Ihanda na Masenha zilizopo Tarafa za Mlali na Zoissa ambapo amepongeza kwa dhati jitihada zilizofanywa na viongozi wa ngazi ya Wilaya na Maeneo hayo.
Aidha Dkt. Msonde alizungumza na baadhi ya Wananchi na kuwasisitiza umuhimu wa kuwapeleka shule watoto wao na kwamba wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanapaswa kuripoti shuleni Siku ya kwanza yaani Januari 09, 2023.
Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Dodoma Bwana Gift Kyando amewaasa wananchi kupeleka watoto wao shule iIi kujenga jamii bora yenye Amani.
Ziara hiyo ya Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Enock Msonde ilihusisha Viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, Mkurugenzi Mtendaji Wilaya Dkt. Omary Nkullo na baadhi ya wakuu wa Divisheni na vitengo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.