Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Mayeka Simon Mayeka ametatua mgogoro baina ya mwekezaji na wachimbaji wa madini katika mgodi uliopo katika Kijiji cha Iduo.
Akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama Mhe. Mayeka amekutana na makundi ya wachimbaji pamoja na uongozi wa Kata ya Iduo ambapo amesisitiza upelelezi ufanyike kubaini ukweli juu ya chanzo cha mgogoro uliotokea baada ya kijana ambaye alipigwa na mlinzi wa mgodi huo akishutumiwa kutorosha madini hali iliyopelekea vurugu mgodini hapo.
Aidha DC Mayeka amekemea vikali kitendo cha wachimbaji madini kujichukulia sheria mkononi akigusia tukio la wachimbaji kumnyang'anya silaha mlinzi wa mgodi huo na kwenda kuvamia nyumba ya mwekezaji na kufanya uharibifu wa mali na kueleza kuwa kitendo hicho ni uvunjaji wa sheria na hakikubaliki.
Mheshimiwa Mayeka pia amekemea suala la utoroshaji wa madini kuwa lilaweza kupelekea kufungwa kwa leseni ya mwekezaji na kusababisha upotevu wa mapato na kuwataka wachimbaji na mwekezaji kila mmoja kwa nafasi yake kutambua mipaka yake katika kazi ili kudumisha amani.
Pamoja na hayo mhe. Mayeka amemuagiza mwekezaji kujenga choo, afisa madini kusimamia usalama wa machimbo hayo na Afisa mazingira Wilaya ya Kongwa kuhakikisha uwepo wa vyoo bora kabla ya kufungua machimbo hayo ya madini ambayo yalifungwa baada ya kutokea kwa vurugu hizo.
Nae Diwani wa kata ya Iduo Mhe. Valentino Seng'unda amewataka wachimbaji wa madini wanaotoka kijiji cha Chamkoroma kutambua na kuheshimu uongozi wa Serikali ya Kijiji na kuwataka waache uchochezi na wafanye kazi kwa utaratibu na kupata riziki ya halali.
Akizungumza baada ya kikao, Afisa mazingira Wilaya ya Kongwa Bw. Godfrey Mujairi amesema Wilaya ya Kongwa ina maeneo makubwa ya kuchimba madini lakini mapato yake yapo chini kutokana na utoroshaji wa madini hayo, hivyo amewaomba wachimbaji na wawekezaji kutii sheria na taratibu za uchimbaji madini.
Akielezea mazingira ya vurugu hizo mwekezaji wa mgodi huo wa madini Bwana Hussein Mohamed amesema mlinzi alimkamata mchimbaji mdogo (ndugu Given Samson mkazi wa Chamkoroma ) akitorosha madini usiku mnamo saa 9 usiku na kuamua kumuadhibu kwa kumpiga na kumsababishia majeraha hivyo baada ya tukio hilo wachimbaji wengine waliamua kumpora mlinzi silaha ambayo aliifatilia na kuikabidhi katika kituo cha Polisi mlali lakini baada ya hapo wachimbaji hao walivamia nyumbani kwake na kufanya uharibifu.
Mpaka kufikia mwisho wa kikao hicho wachimbaji wawili wakazi wa Chamkoroma ndugu Perezi Maduwilu na Juma Mpemba wanashikiliwa na jeshi la Polisi kwa upelelezi zaidi kwa kusababisha uvunjifu wa amani na utoroshaji wa madini mgodini hapo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.