Na Stephen Jackson, Kongwa.
Kamati ya Fedha uongozi na Mipango Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma Imewataka viongozi wa vijiji na Kata kusimamia kikamilifu urejeshwaji wa fedha za serikali zilizotolewa kwa wajasiriamali kupitia mikopo itokanayo na asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe . White Zuberi Mwanzalila, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhe. Richard Mwite ambaye ni Diwani wa Kata ya Mkoka, ameviagiza vikundi vyote ambavyo havijarejesha fedha kufanya hivyo kabla ya Tarehe 31 Oktoba, 2022.
Kamati hiyo chini ya Mhe. Mwite ilitoa agizo hilo wakati wa ziara ya siku mbili ya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa Wilayani Kongwa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Maamuzi hayo yanafuatia baada ya vikundi hivyo kushindwa kufanya marejesho ndani ya muda wa mkataba, ambapo kwa mujibu wa kanuni, vikundi hutakiwa kurejesha fedha katika kipindi cha miezi kumi na mbili.
Aidha kamati ilisikitishwa na taarifa kutoka taarifa ya Afisa Mtendaji Kata ya Sagara Bwana Abdunasil Mboya kudai kuwa baadhi ya wanakikundi wa kikundi cha Furaha kilichopo Kata ya Sagara, wametoroka na fedha za kikundi, hivyo kamati imemtaka Afisa huyo kuhakikisha wanakikundi hao wanapatikana na kurejesha fedha.
Katika ziara hiyo Vikundi mbalimbali vilitembelewa Ikiwa ni pamoja na Furaha kutoka Kata ya Sagara na Upendo kutoka Kata ya Chiwe ambavyo Kila kimoja kilikopeshwa shilingi 4,000,000.00 ambapo kikundi cha Furaha kilikuwa kikidaiwa1,935,000.00 wakati kikundi cha Upendo kikidaiwa shilingi 2,890,000.00 hadi siku ya ukaguzi.
Wakati huo huo Kamati ilipongeza jitihada za kikundi cha Omega Cha Vijana wa boda boda Kata ya Sagara na kikundi cha Nguvu kazi - Vijana kilichopo Kata ya Chiwe kinachoendesha kilimo cha umwagiliaji kwa mkopo wa shilingi milioni tano, ambapo kwa mujibu wa uongozi wa kikundi hicho, vijana hao huzalisha mboga mboga serikali na kusambaza katika masoko ya ndani na nje ya Mkoa wa Dodoma.
Bibi Doricus Ndugai Mwenyekiti wa kikundi cha Upendo alidai kuwa, kutokana na hali mbaya ya hewa kikundi kilipata hasara baada ya kushindwa kuendesha shughuli zake, hivyo Ili kutekeleza agizo la kamati wanakikundi wanalazimika kugawana deni hilo na kuhakikisha wanarejesha fedha kabla au ifikapo Tarehe 31 Oktoba, 2022.
Katika hatua nyingine Kamati ilifanya ukaguzi wa jengo la zahanati ya Kijiji cha Majawanga ambapo linalojengwa kwa nguvu za wananchi linalokadiriwa kuwa na thamani ya Shilingi 60,000,000.00 pindi litakapokamilika.
Katika ukaguzi huo Kamati ilipongeza wananchi na viongozi hao kwa ushirikiano wa dhati wa kuchanga fedha na kuanzisha ujenzi.
Katika taarifa yao wananchi hao walivainisha sababu zilizowasukuma kulingana na kuanzisha ujenzi huo kuwa ni kutokuwepo huduma za Afya katika maeneo ya karibu, hali inayowalazimu kufuata huduma hizo maeneo ya mbali.
Kwa kauli Moja kamati iliunga mkono jitihada hizo na kuahidi kushirikiana na wananchi wa Majawanga kukamilisha ujenzi wa Zahanati hiyo.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kata ya Sagara, kikundi cha Furaha tayari kimeanza kurejesha fedha wanazodaiwa ingawa baadhi ya wanakikundi bado hawajapatikana.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.