Na Stephen Jackson
Wafanyakazi wa Halmashauri ya Kongwa wamempongeza Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala Bibi. Rosemary Iressa kwa kusimamia zoezi la upandishaji vyeo kwa watumishi wenye sifa katika Idara zote za Halmashauri na kuhamasisha watumishi kujiendeleza kielimu.
Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 29/06/2021 majira ya saa nne Asubuhi wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa.
Akizungumza katika kikao hicho cha Tathmini ya upandishaji vyeo kwa mwaka 2020/2021 Bibi Iressa ameeleza kuwa Jumla ya watumishi 587 wa Idara mbalimbali wamethibitishwa kupanda vyeo na miongoni mwao, 295 wamepata mshahara mpya na waliobaki wanatarajia kupata mishahara mipya mwezi Julai 2021.
Kiongozi huyo, ametumia muda mwingi kufafanua na kuwaelekeza watumishi namna ya kusimamia haki zao ili kuzipata kwa wakati. Miongoni mwa mambo aliyotilia mkazo ni pamoja na watumishi kujiendeleza kielimu kwa wakati, na kuhakikisha taarifa zao za kiutumishi zinakuwa sahihi kwenye mifumo.
Katika kikao hicho watumishi wamepata fursa ya kuchangia Agenda mbalimbali, kuuliza maswali na kujibiwa kikamilifu.
Ndugu Elias Chilemu ambaye ni Mratibu wa TASAF Wilaya ya Kongwa, yeye amekielezea kikao hicho kuwa ni cha pekee kwa kuwa ni cha kwanza kufanyika katika kipindi cha miaka kumi (10) ya utumishi wake. ‘’Nina miaka kumi sijawahi kuona kikao kama hiki’’ amesema Elias Chilemu.
Kuelekea hitimisho la kikao hicho Mkuu huyo wa Idara ya utumishi na Utawala ameeleza kuwa Halmashauri ya Kongwa Inatarajia kupokea watumishi 101 wa Ajira mpya wa kada mbalimbali kuanzia tarehe 1 Julai 2021.
Katika kikao hicho mambo mengi ya kiutumishi yamejadiliwa ikiwa ni pamoja na kuichambua hotuba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Tarehe 01/05/2021 katika maadhimisho ya siku ya wafanya kazi (Mei mosi).
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.