Na Bernadetha Mwakilabi
Habari – Kongwa DC
Wasimamizi wa huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa wamepatiwa mafunzo ya udhibiti na utenganishaji takataka zitokanazo na huduma za Afya (TAZIHA) kwa kusudi la kuwajengea uwezo wa kusimamia taka hizo ili zisiweze kuleta athari za kimazingira na kiafya.
Mafunzo hayo yametolewa mwishoni mwa juma lililopita ikiwa ni sehemu ya kutekeleza agizo la Mkurugenzi Mtendaji wa Ustawi wa Jamii na Lishe Tamisemi Dkt. Rashid Mfaume alipotembelea Wilaya ya Kongwa ambapo aliagiza kutolewa mafunzo hayo kutokana na changamoto alizozibaini za usimamizi hafifu wa TAZIHA na matumizi ya maji safi na usafi wa mazingira.
Nae Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dkt. Thomas Mchomvu wakati akifunga mafunzo hayo licha ya kuagiza vituo vya afya kununua vifaa vya kufanyia usafi lakini pia amewataka watumishi wa afya wote kusoma mara kwa mara miongozo ya Wizara ya afya ili iwasaidie katika utendaji kazi wao kwa kulinda afya na mazingira pamoja na kufanya ajenda ya usimamizi wa taka na unawaji mikono kuwa ya kudumu katika kila kikao.
Dkt. Mchomvu ameeleza kuwa ukusanyaji, utenganishaji na usafirishaji wa Taziha ni changamoto katika vituo vya kutolea huduma za afya Wilayani Kongwa kutokana na watumishi wengi waliokuwa na uzoefu wa usimamizi huo kustaafu na waliopo kazini asilimia kubwa kuwa ni wageni walioajiriwa miaka ya karibuni.
Nae Bw. Nelson Rumbeli, Afisa Afya Mkoa wa Dodoma na mkufunzi katika mafunzo hayo ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la utoaji huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini, jambo linalopelekea kuwepo kwa uzalishwaji wa taka kwa kiasi kikubwa hivyo ni vyema watumishi watambue namna ya kuzitunza taka hizo ili zisilete athari.
Vilevile Bw. Rumbeli ameongeza kuwa kumekuwa na changamoto katika vituo vya afya zinazopelekea ugumu katika utenganishaji wa taka hizo ikiwemo uelewa mdogo na usimamizi hafifu wa taka katika vituo, kutokuwepo kamati za kusimamia utenganishaji taziha, vituo vya afya kutokuwa na mizani ya kupimia taziha pamoja na vituo vya afya kutokuwa na takwimu za Taziha.
Pamoja na hayo, Afisa Afya Wilaya ya Kongwa Bw. Mdasilu Bashiru amesema kuwa usimamizi wa Taziha unakabiliwa na changamoto ya usimamizi hafifu wa taka, kutokuwepo kwa takwimu sahihi za ukusanyaji taka na uhaba wa vichomea taka ambapo katika vituo vya kutolea huduma za afya 72 ni vituo vya afya 6 na zahanati 6 zenye vichomea taka vya kisasa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.