Na Stephen Jackson, Kongwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel amewataka wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi ya GS Contractors kuzingatia tahadhali za Afya na usalama mahali pa kazi ili kukuza tija kupitia utekelezaji wa shughuli za Maendeleo.
Mhe. Mwema amesema hayo tarehe 2 Septemba, 2022 wakati alipofanya mazungumzo na wafanyakazi wa kampuni hiyo wakati akikagua ujenzi wa daraja la Makawa lenye urefu wa mita 31.9 linalounganisha kijiji cha Makawa na Mageseni.
Wafanyakazi hao waliojawa na furaha walieleza kuwa kwa sasa hawana mgogoro na mkandarasi isipokuwa wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vifaa vya usalama Mahali pa kazi ikiwemo "mask" na kofia ngumu hali inayowaweka kwenye mazingira hatarishi.
Kufuatia changamoto hiyo Mkuu wa Wilaya Mhe. Remidius Emmanuel amewashauri wafanyakazi wa kampuni hiyo kuchukua tahadhali Kwa kutunza usalama wa Afya zao wakati wa utekelezaji mradi na hivyo kutoa Maelekezo kwa Meneja wa "TARURA" Wilaya ya Kongwa Mhandisi Peter Johnson kuhakikisha Mazingira yanakuwa rafiki kwa Afya za wafanyakazi hao.
Hata hivyo, mradi huo umekuwa Neema kwa wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo utoaji wa Ajira na furasa za Mafunzo kwa vijana akiwemo mwanachuo Irene kutoka chuo cha ufundi Arusha, anayefanya Mafunzo ya vitendo katika mradi huo.
Akizungumza eneo la mradi, mwanachuo Irene ameeleza kunufaika na mchakato wa ujenzi wa daraja hilo kwani umemuwezesha kujifunza stadi mbalimbali za ujenzi kwa kuwa ni mara yake ya kwanza kufanya mafunzo kwa vitendo kuhusu ujenzi wa aina hiyo.
Mradi huo wenye thamani ya Shilingi 598,000,000.00 unatekelezwa na kampuni ya GS Contractors na kusimamiwa na Mamlaka ya barabara mijini na vijijini (TARURA) Wilaya ya Kongwa ukilenga kuunganisha wakazi wa kijiji cha Makawa na Mageseni ambao wamekuwa wakikabiliwa na adha ya usafiri kwa muda mrefu.
Mhe. Mwema amehitimisha ziara yake Kwa kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa Kijiji Cha Silale chenye vitongoji viwili na kuwaahidi kutenga muda wa kufika na wataalamu mbalimbali siku chache zijazo ili kwa pamoja waweze kuzitafutia kero hizo ufumbuzi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.