Wafugaji katika Kata ya Sejeli wilayani Kongwa wameiomba Serikali kuingilia kati suala la wizi wa mifugo unaoendelea katika Kata hiyo hali inayowapa hofu na kukatisha tamaa katika shughuli hiyo.
Wakiongea mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Mayeka Simon Mayeka ambaye pia ni Mwenyekiti wa ulinzi na usalama wilaya wamesema kuwa pamoja na changamoto za malisho, maji, majosho, wataalam na masoko lakini kumekuwa na changamoto kubwa ya wizi wa mifugo kama Ng'ombe na Mbuzi ambapo mfugaji mmoja anaweza kuibiwa hadi mara tatu mfululizo hivyo wanaomba nguvu ya ulinzi na upelelezi, ili kuwabaini wezi wa mifugo hiyo ili waweze kufanya shughuli zao za ufugaji kwa amani na uhuru.
Aidha, wakitoa kero zao, wafugaji hao wameeleza kuwa wizi wa mifugo ni changamoto kubwa inayowakabili wafugaji na inapelekea kwa wingi wao kuogopa kufuga sababu hata ulinzi wa sungusungu wanaowatumia hausaidii kwani inasadikika kuwa sungusungu hao wamekuwa wakitoa siri za wafugaji na kupanga mipango ya wizi.
Sambamba na hayo wafugaji hao wameweka wazi kuwa wanaomba utaratibu wa utoaji vibali urejee ule wa awali yaani kibali kitoke Kijiji ambacho mfugo unatoka kwenda mnadani na kutoka mnadani kwenda kijiji ambacho mfugo unaenda ili kuendelea kuwabana wezi wa mifugo kwani vibali kwa Sasa vinatolewa mnadani tu.
Awali ya yote kabla ya kutoa majibu juu ya malalamiko hayo Mhe. Mayeka alitumia wasaa huo kuendesha kura ya siri kwa wafugaji kupiga kura kuwabaini wezi wa mifugo kwa majina na nafasi zao ili kuwachunguza na kuwachukulia hatua zaidi pindi watakapopatikana na hatia ya makosa ya wizi wa mifugo.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa mhe. Mayeka S. Mayeka akitolea ufafanuzi hoja zilizoibuliwa kwenye kikao.
Vilevile Mhe. Mayeka ametoa mikakati ili kudhibiti wizi huo ikiwemo kuweka kizuizi (Barrier) kwaajili ya kukagua magari yanayotoka wilaya ya Kongwa kwenda wilaya za jirani, na kuwataka wananchi kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji husika kuweka doria ya sungusungu kwa kuwatumia Askari wa Jeshi la Akiba ambao ni waaadilifu ili kulinda maeneo yao.
Diwani wa Kata ya Sejeli Mhe. Chilingo Ng’hambi Chimeledya akiongea na wananchi wa Kata ya Sejeli katika kikao
Licha ya kuwataka wananchi kutokujichukulia sheria mkononi pindi watakapowabaini wezi hao lakini amewataka wafugaji na wananchi kushirikiana kwa pamoja kutokomeza wizi wa aina yoyote na wizi wa mifugo kwani wezi wakitawala ufugaji utakuwa mgumu na ametoa rai kwa wananchi kutoka kila Kijiji ndani ya Kata wanapofanya vikao, ajenda kubwa iwe ya usalama.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.