Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Kongwa Bi Magreth Temu amekabidhi baiskeli 35 kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Banyibanyi wanaotembea umbali mrefu kwenda shule kutokea Kijiji cha Mkutani takribani kilomita Saba.
Baiskeli hizo zilizokabidhiwa ni sehemu ya ufadhili kutoka kwa Wahandisi wasio na Mipaka kutoka Marekani (USA Engineers without borders) zikiwa na lengo la kuondoa vikwazo na changamoto za elimu zikiwemo utoro unaotokana na kutembea umbali mrefu kwa wanafunzi wa shule za Sekondari.
Akiongea wakati wa kukabidhi Baiskeli hizo Bi Temu ametoa shukrani kwa Wahandisi wasio na Mipaka kwa kusukuma gurudumu la elimu katika Wilaya ya Kongwa kwani licha ya baskeli hizo wameweza kujenga nyumba ya mwalimu, matundu ya vyoo 12, miundombinu ya kuvunia maji na chumba cha kompyuta kwaajili ya kusaidia wanafunzi kusoma masomo ya Tehama katika shule ya msingi Mkutani ambapo ameongeza kwa kuwa baiskeli hizo ziwe chachu ya kuongeza bidii ya masomo kwa wanafunzi.
Aidha Mwl. Magreth Temu ameshukuru viongozi wa wilaya ya Kongwa hususani Mbunge wa Jimbo la Kongwa Mhe. Job Ndugai kwa kutoa kipaumbele kwa wanafunzi wanaotoka Kijiji cha Mkutani kupata baskeli hizo kwani ni wanafunzi wa maeneo mengi wanahitaji msaada huo na kuwataka wazazi kuhakikisha wanazitunza baiskeli hizo ili ziwe na faida iliyokusudiwa.
Pamoja na kuhimiza uchangiaji wa Lishe mashuleni pia Mwl. Temu amewataka wanafunzi wote waliofeli mtihani wa darasa la saba mwaka 2024 kurudia darasa la saba mwaka 2025 ili kuendelea na masomo, na kuwasihi wazazi kujitokeza kuwaandikisha shule wanafunzi wenye ulemavu ili nao wapate elimu.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Hogoro Mheshimiwa Mtwanga Sadala amewataka wenyeviti wa vitongoji kushirikiana na wazazi kushughulikia utoro wa wanafunzi mashuleni na kuwasihi wanafunzi kuwa na nidhamu kwa walimu na jamii yote kwa ujumla.
Akiongea kwa niaba ya wanafunzi waliopokea baiskeli hizo, Claudia Njijila mwanafunzi wa shule ya Sekondari Banyibanyi amesema awali walipata shida ya kutembea umbali mrefu jambo lililopelekea wao kuchoka na kushindwa kusoma vizuri lakini baiskeli zitawasaidia kuwahi shule na kupata muda mzuri wa kujisomea.
Kwa upande wao wazazi wa wanafunzi hao wamesema kuwa awali walipata adha kubwa na walitakiwa kudamka saa 10 usiku ili kuwasindikiza watoto wao kwenda shule, hivyo wanashukuru Wahandisi wasio na Mipaka kutoka Marekani kwa msaada huo.
Akiongea kuwakilisha jumuiya ya Shule,Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mkutani, Samwel Chidabile amesema anashukuru Wahandisi wasio na Mipaka kwani wamekuwa ni marafiki bora tangu mwaka 2017 walipofanya shughuli za kuboresha miundombinu ya shule hiyo na mpaka sasa wamepokea baiskeli 121 ambazo zinasimamiwa na kamati ya shule kuhakikisha zinakuwa salama na kutumika kwa wanafunzi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.