Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa na Diwani wa Kata ya Kongwa Mhe. White Zuberi amewaahidi wanachuo wa Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) Kongwa kuwa watapatiwa fursa ya kushiriki katika ujenzi wa majengo yote ya karibu yanayojengwa na Halmashauri ili kuwawezesha kufanya mafunzo yao kwa vitendo.
Mhe. Zuberi ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya pili ya fani ya uhazili na kompyuta katika Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) Kongwa ambapo ameeleza kuwa wanachuo hao watashiriki kufanya mafunzo kwa vitendo katika majengo ya Serikali ili watakapomaliza chuo wawe mafundi bora na mahiri.
Vilevile Mhe. Zuberi amewatia moyo wahitimu na kuwasihi waone fahari juu ya ujuzi walioupata kwani una tija kwa jamii na utawawezesha kujiajiri na kupata elimu ya juu zaidi hivyo watumie ujuzi huo kwa kuanzisha vikundi, kubuni miradi ya maendeleo na kuunda vikundi vya vijana ambavyo Halmashauri itavipatia fedha za 10% kwaajili ya kuendesha miradi.
Aidha Mhe. Zuberi amefafanua kuwa kwa changamoto ya upatikanaji wa leseni za usafiri, Halmashauri itawasiliana na ofisi ya mapato TRA ili waweze kuweka mfumo rahisi wa utoaji leseni ndani ya Wilaya ili wanachuo hao wanapomaliza mafunzo yao waweze kupata leseni hizo kiurahisi bila kwenda Mkoani.
Mgeni rasmi katika mahafali Mhe. White Zuberi akitoa neno kwa wahitimu
Mkuu wa chuo cha VETA Kongwa Bwana Abdulkadir Yusuff ameshukuru Serikali kwa kuwapatia vifaa katika fani za uhazili, kompyuta, ushonaji na uwashi na kukiri kuwa kupitia chuo hicho wafanyabiashara watanufaika kwa kuuza vifaa vya ufundi na wananchi kupata huduma bora na rahisi kupitia wahitimu wa chuo hicho.
Licha kutaja changamoto za ukosefu wa vifaa katika fani za useremala na ufundi magari, upungufu wa mashine za kuchapa, upungufu wa vitendea kazi katika karakana na ofisi za walimu, ukosefu wa karakana ya uhazili na kompyuta, upungufu wa mabweni lakini Mwl. Yusuph amesema kuwa chuo kinaendelea kutekeleza wajibu wake wa kutoa mafunzo.
Mkuu wa chuo cha VETA Kongwa akiongea wakati wa mahafali hayo
Kwa upande wao wahitimu hao 11 wameshukuru na kupongeza Serikali ya awamu ya sita, uongozi wa chuo pamoja na wakufunzi wao kwa elimu waliyoipata na kueleza kuwa wamefanikiwa kupata ujuzi mahiri wa nadharia na vitendo utakaowawezesha kufanya kazi maeneo mbalimbali hivyo wapo tayari kutumikia Taifa kwa ujuzi waliopata.
Aidha katika Risala yao wahitimu hao wameomba Serikali kujenga maktaba yenye vitabu vya kujifunzia, na kuomba kila muhitimu kupewa vifaa vya kuanzia kufanya kazi kulingana na fani yake ili kujenga dhana kamili ya kujiajiri.
Wahitimu wakisoma risala mbele ya mgeni rasmi.
Baadhi ya fani zinazotolewa katika Chuo cha mafunzo ya Ufundi stadi VETA Kongwa chenye jumla ya wanafunzi 245 ni pamoja na uhazili na kompyuta, umeme wa magari majumbani na viwandani, ujenzi, uwashi, seremala, udereva wa magari na pikipiki na fani ya ushonaji.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.