Na Mwandishi Wetu, Kongwa DC
Wananchi wa Kijiji cha Tubugwe Kibaoni Kata ya Chamkoroma Wilayani Kongwa, wamehofia kuchimba kwa mikono mabwawa ya Kufugia samaki katika mradi wa shamba darasa la ukuzaji wa Viumbe maji.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 119 umepangwa kutekelezwa kiwilaya na Wizara ya Mifugo na uvuvi katika Kijiji cha Tubugwe Kibaoni kama Kituo maalumu cha kujifunzia stadi za ukuzaji wa Viumbe maji.
Wakijadili katika mkutano wa hadhara Januari 17, 2023, Wakazi wa Kijiji hicho waliazimia kutumika kwa zana za kisasa kutekeleza mradi huo kwani lengo lao ni kupata mradi wenye tija na si kunufaika na fedha za utekelezaji mradi.
Akitolea ufafanuzi kuhusu mradi huo, Afisa Mifugo Wilaya ya Kongwa Bwana Msafiri Mkunda, alitaja faida za mradi huo kuwa ni pamoja na kuwapatia lishe bora na kuongeza kipato kwa wananchi kwani mradi utafungua fursa za kibiashara kutokana na wananchi wa Maeneo mbalimbali kuingia Kijijini hapo kupata mafunzo.
Bwana Mkunda ameitaka jamii kushiriki katika utekelezaji wa mradi huo Ili uweze kukamilika kwa wakati.
Maamuzi hayo ya Wananchi yamefikiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Januari 17, katika Ofisi ya Kijiji hicho.
Awali Mhandisi wa Mradi huo Bi. Anitha Kalumuna alieleza ukubwa na kina cha mabwawa ili kujenga uelewa wa wananchi ambapo aliwataka wananchi kutaja mbinu watakayotumia Ili kuzingatia viwango vya Kitaalamu.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa Kitengo cha Manunuzi, Afisa Manunuzi Bwana Samwel Mwamalange, ameitaka kamati itakayoteuliwa kusimamia mradi, kuhakikisha inafuata Sheria na taratibu za utekelezaji wa miradi ya Serikali.
Majadiliano hayo ya kina baina ya Wananchi kuhusu utekelezaji wa mradi yamefikia hitimisho kwamba Kamati ya usimamizi itashughulikia upatikanaji wa Mitambo ya kuchimba mabwawa hayo na wananchi watashiriki kwenye shughuli nyingine kama itakavyoelekezwa.
Uamuzi huo wa wananchi ulikuja baada ya Divisheni ya mifugo kuwapa Uhuru wa kujadili kwenye mkutano wa hadhara jinsi ya kutekeleza mradi huo hususani kwenye uchimbaji wa mabwawa.
Katika mradi huo uliotengewa kiasi cha shilingi milioni 119, jumla ya mabwawa manne yaliyofuatana na yenye vipimo sawa yanatarajiwa kuchimbwa, sambamba na miundombinu mingine iliyoainishwa kwenye mchanganuo wa mradi.
Mkuu wa Divisheni ya Mifugo na Uvuvi Bwana Msafiri Mkunda akitoa ufafanuzi katika mkutano wa hadhara, Januari 17, 2023.
Mhandisi wa Mradi Bi. Anitha Kalumuna akifafanua vipimo vya Kitaalamu vya mabwawa ya Kufugia samaki.
Afisa Manunuzi Bwana Samwel Mwamalange akielezea mambo ya kuzingatia wakati wa utekelezaji mradi
Mmoja wa wasimamizi wa mradi kutoka Kijiji Cha Tubugwe Kibaoni akichangia mada.
Baadhi ya Wananchi wa Kijiji Cha Tubugwe Kibaoni wakiwa kwenye Mkutano wa hadhara kuhusu uchimbaji wa mabwawa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.