Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka S. Mayeka amefanya kikao cha dharura na wajumbe wa huduma ya Afya ya Msingi ili kujadili mlipuko wa kipindipindu Wilayani Kongwa. Kikao hicho kimetokana na ongezeko la wagonjwa ambao wamefika katika vituo vya Afya na makambi ya dharura kwa ajili ya kupatiwa huduma.
Akizungumza wakati akieleza hali ya ugonjwa huo kwa Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dr. Thomas Mchomvu, ameeleza kuwa mpaka wakati wa kikao hicho kumeripotiwa kuwa na wagonjwa 71 na kati ya hao wagonjwa 51 wameshatibiwa na wamepata nafuu na kuruhusiwa. Wagonjwa waliobaki wanaendelea kupata huduma na wataruhusiwa karibuni. Aidha Dkt. Thomas ameeleza kuwa zaidi ya asilimia 95 ya wagonjwa walipata kipindupindu baada ya kuhudhuria mazishi yaliyofanyika tarehe 14 mwezi wa kumi katika Kijiji kinachopatikana Gairo ambapo walikula na kunywa katika msiba huo.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dr. Thomas Mchomvu akieleza hali ya mlipuko wa Ugonjwa wa Kipindupindu katika Wilaya ya Kongwa.
Mganga Mkuu ameeleza kuwa ili kuthibitisha mlipuko wa ugonjwa kitaalamu ni lazima vifanyike vipimo vya sampuli tofauti na sampuli zote kumi na saba zilibainisha kuwa kuna vimelea vya ugonjwa huo, lakini pia sampuli tatu zilipelekwa Dodoma kwenye hospitali ya rufaa ya Mkoa kwa ajili ya uhakiki zaidi na majibu pia yalitoka kuwa sampuli zina vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu.
Aidha Dkt. Thomas ameainisha mbele ya Mkuu wa Wilaya gharama za kupambana na ugonjwa huo kuanzia tarehe 16 mpaka wakati wa kikao, zimeshatumika takribani milioni nane kwa ajili ya vifaa, dawa Pamoja na gharama nyingine za matibabu hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka S. Mayeka akiongea na wajumbe wa Huduma ya Afya ya Msingi.
Akiongea kabla ya kuhitimisha kikao, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka S. Mayeka ametoa maagizo maalumu Pamoja na kutilia mkazo maazimio ya kikao hicho ikiwa ni Pamoja na kusitishwa magulio, sherehe, vigodoro kwa muda wa wiki mbili na katazo la huduma ya vyakula katika misiba na mikutano ya kidini kwa muda wa wiki mbili katika kata nne ambazo zimeathiriwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu. Kata hizo ni Mlali, Chamkoroma, Ngh’umbi na Chiwe. Maadhimio mengine ni kusimamia usafi wa vyoo na kuhakikisha kaya zinatumia vyoo, Pamoja na kuhakikisha shule zinasimamia usafi wa vyoo ipasavyo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.