Na Bernadetha Mwakilabi, Kongwa.
Viongozi wa Halmashauri ya wilaya Kongwa wameshauriwa kuweka msisitizo mkubwa kutoa elimu kwa wakulima kujisajili katika ruzuku ya mbolea ili kuisaidia Serikali kupata takwimu ya wakulima na mashamba wanayolima.
Ushauri huo umetolewa na mshauri wa Serikali za mitaa Bwn. Nathalis Linuma kwa madiwani na wataalam mbalimbali katika mkutano wa baraza la madiwani wa robo ya nne ya mwaka 2021-2022 uliojumuisha wananchi.
Amesema kuwa takwimu hiyo itasaidia pia Serikali kujua kiasi gani cha mbolea na mbegu kinahitajika kuwapatia wakulima wake kuwasaidia kulima kilimo Bora cha kisasa na chenye tija kuondokana na janga la njaa.
Pamoja na hayo mshauri huyo amesema kuwa katika kila mikutano ya vijiji viongozi waibue mafanikio mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao kama miradi ya Afya na elimu pia kutolea ufafanuzi suala la kufuta utoro mashuleni.
Naye mheshimiwa Richard Mwite Diwani wa kata ya Mkoka alipokuwa akichangia hoja ya wimbi kubwa la vijana kujiua kutokana na ugumu wa maisha amevitaka vikundi vilivyokopa fedha za halmashauri za vijana akinamama na walemavu kurudisha kwa wakati fedha hizo ili vikundi vingine vikopeshwe.
Naye Bi Joyce Ibrahim Mkaugala katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya akichangia hoja hiyo amesema kuwa kuna haja kubwa kwa vijana kupewa elimu na ushauri wa kujitambua na kuanzisha fursa nje ya kuajiriwa kwa kuanzisha vikundi mbalimbali vya ufugaji kilimo na Biashara.
Aidha bi. Joyce ameiomba mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi katika maeneo yao juu ya mabadiliko ya Sheria ya tozo na umuhimu wa tozo mbalimbali ili kuepusha malalamiko ya wananchi kwa Serikali.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri Dr Omary Nkullo ameahidi kufanyia kazi mambo yote yaliyoshauriwa na kujadiliwa katika mkutano huo ili kuleta tija kwa wananchi na Serikali kwa maendeleo ya nchi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.