Walimu wanufaika wa nyumba zilizojengwa na mfuko wa maendeleo ya Jamii Tasaf wameaswa kuzitunza nyumba hizo na kuhakikisha zinakuwa katika mazingira mazuri na nadhifu ili mradi huo uwe wenye tija katika shule ya sekondari Chitego.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo katika hafla ya kukabidhi nyumba za walimu katika Kata ya Chitego. Dkt Nkullo pia amempongeza na kumshukuru mbunge wa jimbo la Kongwa Mhe. Job Ndugai kwa kuhakikisha anapambana usiku na mchana ili majengo hayo yanajengwa katika Kata ya Chitego. Pia ameshukuru diwani na timu yake pamoja na watendaji wa kata na vijiji kwa kujitoa kwa dhati kuhakikisha ujenzi wa nyumba hizo unakamilika.
Kabla ya kukabidhi kipaza sauti, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ameeleza kuwa sababu Serikali inatoa fedha nyingi kujenga miradi ya elimu ikiwemo nyumba za walimu na wananchi wamekuwa wakitumia nguvu zao kuhakikisha miradi husika inakamilika, hivyo wananchi hawana budi kuhakikisha kuwa wanahamasisha wanafunzi kutumia fursa za elimu na kujiandikisha na kuhakikisha wanasoma ipasavyo kwani hakuna urithi mwingine wa kumwachia mtoto ila elimu.
Akiongea kabla ya kukabidhi vyeti, Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tasaf Ndg. Salum Mshana ameeleza furaha yake baada ya kukagua mradi na kudai kuwa ukamilishaji umefanyika kwa usahihi na Tasaf ikiwakilishwa na yeye mwenyewe imefurahi kwa mradi kuisha kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.
Akihitimisha ndg. Salum Mshana amefafanua kuwa mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tasaf uko nchi nzima na amewasifu viongozi kwa kupambana kuhakikisha majengo hayo yanajengwa Chitego na yanakamilishwa kwa ukamilifu wake.
Naye Mbunge wa jimbo la Kongwa na Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai ameeleza furaha yake kuona mradi huo umekamilika na umefikia kukabidhiwa kwa wanufaika. Pia amepeleka shukrani zake za dhati kwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mradi huo umefanyika chini ya serikali yake.
Akiongea baada ya kupokea nyumba, Mwalimu wa shule ya sekondari Chitego mwl. Ramadhani Hamza ameeleza furaha yake kukabidhiwa nyumba na ametoa shukrani zake za dhati kwa uongozi wa Wilaya, Kata na Kijiji kwa kuhakikisha mradi huo unakamilika bila kusahau uongozi wa Tasaf ambao wametoa fedha za mradi. Mwl. Ramadhan ameeleza kuwa majengo hayo yanaenda kurahisisha ufanyaji kazi wa walimu muda wowote ikiwemo muda wa usiku lakini pia nyumba hizo zinaenda kuwapunguzia walimu umbali wa kutoka nyumbani Kwenda shule kufundisha.
Naye kiranja mkuu wa shule ya sekondari chitego Goodluck Frank ameeleza furaha yake kuona walimu wake wakipatiwa nyumba hizo karibu na shule na kudai kuwa itarahisisha walimu kuwasaidia wanafunzi muda wa maandalizi ya kujisomea baada ya muda wa kawaida wa shule kuisha kwani changamoto waliyokuwa nayo ilikuwa kupata usaidizi baada ya masomo kuisha na wakati wanajisomea. Pia ameonyesha Imani yake kuwa ufaulu utaongezeka kutokana na uwepo wa majengo hayo kwani wanafunzi wakiwa katika masomo ya usiku watapata usimamizi na usaidizi wa walimu ambao wako karibu na shule.
Aidha Mratib wa Tasaf Wilaya ya Kongwa ndugu. Elias Chilemu ameeleza kuwa takribani shilingi za kitanzania milioni mia moja themanini na nane zimetumika kukamilisha mradi huo na kumshukuru Mhe. Mbunge kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha upatikanaji wa fedha hizo kwa ajili ya mradi. Ndg. Chilemu ametoa rai kwa majengo hayo kuleta tija katika ufaulu wa wanafunzi kwani dhumuni la Tasaf kushiriki katika kuhakikisha mradi huo unakamilika ni ili walimu waweze kuwa na ukaribu na wanafunzi wao kuwasaidia katika muda wa ziada wa masomo ili ufaulu uongezeke.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.