Na Stephen Jackson
KONGWA.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka amewataka wazazi wenye wanafunzi waliopo kwenye madarasa ya mitihani ya Taifa, kuwapunguzia kazi za nyumbani ili kuwapa muda zaidi wa kujisomea.
Mhe. Antony Mtaka ameyasema hayo leo Jumapili Tarehe 08 Mei, 2022 wakati akihutubia waumini wa kanisa la Anglikana Kongwa Dayosisi ya Mpwapwa, katika ibada Maalumu iliyoendeshwa na Askofu wa Dayosisi hiyo Mhashamu Dr. Jacob Erasto Chimeledya. ‘’ Wazazi wote ambao wana watoto waliopo kwenye mitihani ya taifa mwaka huu, shule ya msingi mtihani wa Taifa ni Darasa la nne na darasa la saba. Kidato cha kwanza mpaka cha nne ni "form II" na "Form Four". Wazazi wote ambao wana watoto waliopo kwenye madarasa ya Mitihani ya Taifa wawapunguzie shughuli za nyumbani, watoto wapate muda mzuri wa kufanya maandalizi ya kujisomea.’’ Alitanabaisha Mheshimiwa Mtaka.
Sanjali na hayo Mhe. Mtaka ameziagiza kamati za shule pamoja na wazazi kukutana na kutafuta namna watakavyoweza kuwasaidia watoto hao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanapata chakula Cha mchana shuleni, lengo likiwa ni kuwapa muda zaidi wa kujisomea.
Mheshimiwa Mtaka alizungumza hayo kufuatia matokeo yasiyoridhisha Wilayani Kongwa ambapo alibainisha kuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Spika Mstaafu Mhe. Job Yustino Ndugai anaendelea na ufuatiliaji kuhusu changamoto hiyo.
Katika ibada hiyo Mhe. Mtaka amechangia jumla ya mifuko 100 ya saruji kwaajili ya ujenzi wa ofisi za kanisa hilo pamoja na madirisha sita ya ‘’Alminium’’ kwaajili ya umaliziaji wa jengo la Kanisa hilo la Mtakatifu Michael, Dayosisi ya Mpwapwa.
Ili kufanikisha ujenzi wa kanisa hilo ambalo lipo katika hatua ya umaliziaji , Mheshimiwa Mtaka ameendesha harambee ya kuchangia ujenzi huo unaoendelea kwa viongozi wa chama na serikali walioshiriki ibada hiyo na kufanikisha kupatikana kwa saruji na Madirisha ya vioo.
Kwa upande wake Askofu Jacob Chimeledya kupitia Mahubiri ya ibada hiyo, ametoa wito kwa viongozi wa Serikali ya Tanzania kutokukiri kwa wananchi kuwa nchi yetu ni Nchi maskini kwa kuwa inazo raslimali za kutosha. ‘’Inchi yetu Ina Mali nyingi, hakuna sababu wala haiko sababu ya viongozi wetu wa Tanzania kukiri kwamba sisi tuko Maskini.’’ Alisema Askofu Chimeledya.
Katika Ibada hiyo akinamama wa kanisa hilo wakiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Dr. Faith Mganga walikabidhi gari aina ya ‘’Toyota Noah’’ lenye namba za usajili T479 DZD kwa Mchungaji wa kanisa hilo kwaajili ya huduma za kanisa. Kwa mujibu wa Mwakilishi wa Kampuni ya Fahari Motors waliofanikisha uagizaji wa gari hilo ametaja thamani ya gari hilo kuwa ni Tshs. 19,500,000/=.
Taarifa ya Akinamama hao, inaeleza kuwa fedha za ununuzi wa gari hilo zimetokana na michango yao wenyewe pamoja na wadau mbalimbali, akiwemo Mkuu wa wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Remidius Mwema Emmanuel chini ya usimamizi wa Dr. Faith Mganga, Muumini na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.