Shule 130 za Msingi zilizoandikisha jumla ya wanafunzi 7986 waliofanya mtihani mwaka 2024, zimefanikisha kufaulisha idadi ya wanafunzi 7321 waliofaulu Kwenda kidato cha kwanza, sawa na asilimia 91.67 ambapo imepelekea Wilaya ya Kongwa kupata ongezeko la asilimia 5 ya ufaulu ukulinganisha na mwaka 2023.
Hayo yameelezwa na Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Kongwa Mwl. Magreth Temu katika Kikao maalum cha wadau wa Elimu ikiwemo viongozi wa Serikali, walimu wakuu, ma-afisa elimu Kata kwa dhumuni la kuongea na wanafunzi na wazazi wa wanafunzi waliofeli mtihani wa darasa la Saba mwaka 2024.
Akizungumza mbele ya mgeni rasmi wa kikao hicho Mwl. Magreth Temu ameeleza kuwa mafanikio haya yamepelekea Wilaya ya Kongwa kushika nafasi ya pili katika Mkoa wa Dodoma ambapo ni wanafunzi 665 tu waliofeli mtihani huo na kati yao 466 ni wasichana na 199 ni wavulana, imebainishwa kuwa baadhi ya sababu zilizopelekea wanafunzi hao 665 kufeli mtihani wa darasa la saba ni kujifelisha kwa maksudi na pia wengi wao kushawishiwa na wazazi wao wasifanye vizuri katika mtihani huo wa Taifa.
Mwl. Magreth ameeleza sababu za mafanikio yaliyopatikana, kuwa ni ushirikiano mzuri uliopo baina ya viongozi wa siasa pamoja na wataalam wa Halmashauri uliopelekea ziara za Kwenda katika kila Kata kukemea wanafunzi kujifelisha na kuhamasisha elimu kwa ujumla.
Mwl. Magreth Temu ameeleza pia kuwa ziara za Mbunge wa Kongwa Mhe. Job Ndugai katika Kata zote kusisitiza elimu na kutatua changamoto zote katika elimu pamoja na kuandikishana mikataba kati ya wazazi na shue husika imechangia kwa kiasi kikubwa sana kuinua ufaulu wa wanafunzi.
Aidha ufuatiliaji wa karibu wa Idara ya Elimu na ari ya kufaulisha kwa kiwango cha juu waliyokuwa nayo ma-afisa elimu Kata, walimu wa masomo husika pamoja na walimu wakuu imeongeza ufaulu na ushindani baina ya shule na shule katika Wilaya ya Kongwa.
Kampeni za kuelimisha wazazi na Jamii kuhusu fungu la Halmashauri kusaidia mahitaji kwa wanafunzi waliofaulu na wanaotoka katika Kaya maskini imechangia kwa wanafunzi kutokujifelisha kwa idadi kubwa. Pia Sera mpya inayobainisha kuwa elimu ya msingi ni kuanzia awali hadi kidato Cha nne ambayo inawaruhusu wanafunzi waliofeli mtihani wa darasa la Saba kurudia darasa imeongeza chachu ya wanafunzi kutamani kufika kidato cha nne kwani kwa tathmini, wanafunzi 13 waliorudia darasa na kufanya mtihani kwa mara ya pili, kati yao kuna waliopata wastani A na kwenda shule maalum mwaka 2024
Baadhi ya viongozi walipata wasaa wa kutoa nasaha zao katika kikao ikiwemo Diwani wa kata ya pandambili ambaye ameeleza kwa kina kuwa pasipokuwa na elimu basi maendeleo hayataonekana na kusisitiza kuwa kama wananchi wanataka wapate maendeleo basi lazima kwanza waanze kuzikimbilia fursa za elimu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, dkt. Omary Nkullo amewapongeza walimu chini ya uongozi wa walimu wakuu kwa matokeo mazuri, bila kuwasahau wazazi waliohamasisha wanafunzi kufanya vizuri. Dkt. Nkullo ameongeza kuwa licha ya kuwa na shughuli nyingi za kiserikali, Mbunge wa Jimbo la Kongwa Mhe. Job Ndugai amekuwa akizunguka katika kila Kata kuongelea elimu na kusisitiza umuhimu wa wazazi kuwahamasisha watoto kufanya vizuri katika masomo yao.
Aidha ameongeza kuwa wanafunzi wamepata nafasi ya pili ambayo haikuwepo kipindi cha nyuma na kuwasihi wazazi watumie hii nafasi kuwarithisha elimu watoto wao Ili wapambane katika dunia ya sasa ya Sayansi na teknolojia. Mkurugenzi Mtendaji, pia amewasihi Watendaji kata na vijiji kuhakikisha wanafunzi waliofaulu wanaandikishwa Shuleni Ili kuendelea na masomo yao.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhe. White Zuberi ametoa nasaa zake na kuanza kwa kueleza kuwa kuandaa watoto wa Kongwa kielimu ni kutengeneza viongozi wa baadae ambao wataliletea Taifa maendeleo kwani Taifa linaendelea kwa watu wake kusoma na Serikali Ina nia njema ya kuinua kiwango Cha elimu Cha watu wake.
Aidha Mhe. White Zuberi ameeleza kuwa kwa miaka mingi mkoa ulikuwa haufanyi vizuri lakini amebainisha kuwa Mkuu wa mkoa wa sasa Mhe. Rosemary Senyamule ameunga mkono kwa asilimia mia moja harakati za kunyanyua ufaulu wa wanafunzi katika Wilaya na ndio maana katika kila ziara za Mhe. Rosemary huwa anasisitiza kuhusu elimu na wanafunzi kuandikishwa ili kuunga mkono Juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata elimu ya Msingi.
Mhe. White Zuberi pia amekemea dhana ya wazazi kulaghaiwa na madalali wanaochukua watoto kwenda kufanya kazi za ndani kwani Watoto wengi wanateseka sana na kunyanyaswa na mabinti wengi wadogo wameishia kupewa mimba na kuambukizwa maradhi jambo linalopelekea wao kurudi nyumbani wakiwa hawana kipato chochote, swala ambalo linaongeza utegemezi na umaskini kwenye familia.
Aidha Mhe. White Zuberi ameelezea adhma ya Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kufanikisha wanafunzi si nchini ya 1000 kuendelea na masomo ya chuo kikuu na amefafanua kuwa kwa kulitambua hilo zimetolewa fedha kiasi cha shilingi million 180 kwa dhumuni la kuanzisha shule za bweni zitakazoandikisha wanafunzi waliofanya vizuri. Pia mwenyekiti wa Halmashauri ameelezea maelekezo ya Halmashauri kutenga Fedha za mapato yake ya ndani ili kusomesha watoto wawili wawili (wakike na wakiume) bure kutoka katika kila Kata, dhumuni ni kuinua kiwango cha elimu na ufaulu wa wanafunzi na kuhamasisha wazazi kuona umuhimu wa elimu wa watoto wao.
Akitoa mchango wake Mwl.Megi Chela amewaasa watoto kuchangamkia fursa waliyopatiwa ya kurudia masomo na ameeleza mkutano kuwa watoto waliojifelisha walishaandaliwa madawati tayari kwa kurudia masomo na kufanya mtihani kwa mara ya pili. Aidha Mwalimu Megi amegusia uhusiano mzuri kati ya wanafunzi, walimu na wazazi kuwa chachu ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu katika Wilaya ya Kongwa.
Akiongea kabla ya kuhitimisha kikao, Mbunge wa jimbo la Kongwa Mhe. Job Ndugai ameeleza wadau kuwa kati ya mambo muhimu Serikali inayopigania ni elimu kwa wananchi wake na ndio maana katika Wilaya ya Kongwa zimejengwa shule za kutosha katika kila Kata ili wanafunzi wapate elimu karibu na makazi yao. Mhe. Job Ndugai ameeleza kuwa dunia inaelekea katika matumizi makubwa ya teknolojia hivyo kukosa elimu katika kipindi hiki ni kujinyima haki ya msingi ya kufaidi fursa nyingi ulimwenguni.
Licha ya kuwataka wanafunzi kurudi shuleni, Mhe. Ndugai amewahoji wanafunzi mmoja mmoja na wazazi wao na kuwataka wamuahidi kuwa watarudi shule kurudia masomo yao na wakafanya hivyo huku wazazi wakiahidi kuwahimiza Watoto wao katika masomo na kurudi shule ili kupata elimu.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.