Wananchi wa Kata ya kibaigwa wameiomba Serikali kupanua barabara katika eneo la katikati ya mji ili kuchochea ufanisi katika ufanyaji wa biashara, kupata egesho zuri la magari hususani malori na kuboresha eneo la gulio hali itakayokuza uchangiaji wa mapato.
Wananchi hao wameyasema hayo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka alipotembelea Shule ya Msingi Mzogole iliyopo Kijiji Cha kibaigwa kujionea mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo uliotengewa zaidi ya milioni 103, na kuongea na Wananchi wa Kata ya kibaigwa kujua changamoto zinazowakabili na namna ya kuzitatua.
Akijibu hoja za wananchi hao Mhe Mayeka amemuagiza Meneja TANROAD wilaya kuwasiliana na Meneja wa TANROAD mkoa kuona namna ya kushughulikia suala la utanuzi wa barabara iliyopo katikati ya mji wa kibaigwa kwa upande wa kulia na kushoto ili kurahisisha biashara za wananchi.
Vilevile Mhe. Mayeka S. Mayeka amesema suala la ulinzi na usalama ni jukumu la kila Mwananchi, hivyo madereva bodaboda wawe na uongozi unaotambulika ili wasaidiane na polisi kupata wahalifu na vijiwe vyote vya bodaboda vifahamike na visajiliwe. Pia ametoa rai kwa Jeshi la polisi liendelee na doria na wananchi watoe taarifa za matukio ya kihalifu kabla baada yanapotokea.
Aidha Mhe. Mayeka ametolea ufafanuzi suala la changamoto ya mazingira mabovu ya gulio la kibaigwa na kueleza kuwa Serikali ipo kwenye mpango wa kujenga soko kubwa la Machinga litakalokuwa na mazingira mazuri na rafiki kwaajili ya Wafanyabishara wa Kibaigwa.
Mhe. Mayeka pia amewataka Ruwasa Mkoa na Taifa kuangalia viwango vya malipo ya maji kuwa rafiki kwa wananchi kwani mji wa kibaigwa unakua kwa kasi na maji mengi yanahitajika, na kuhusu suala la kupungua Kwa umeme tayari kituo cha umeme kilichopo mbande kitaanza kufanya kazi muda si mrefu na kuondoa adha hiyo.
Kwa upande wake Afisa maendeleo ya Jamii Wilaya ya Kongwa Bi Paskalina Duwe amewataka wanawake vijana na watu wenye Ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo ya vikundi ya 10% za mapato ya Halmashauri na kuwasihi wakazi wa Kibaigwa kuongeza uaminifu katika urejeshaji wa fedha hizo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.