Wakazi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Kibaigwa, wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na mikutano ya Kliniki ya Ardhi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel wakati alipokuwa akizungumza na Wakazi wa Kibaigwa kwenye Mkutano maalumu wa Kliniki ya Ardhi unaofanyika kwa muda wa siku mbili katika uwanja wa CCM Kibaigwa.
Mhe. Mwema amesema fursa hiyo imetokana na Maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwamba viongozi watoke ofisini na kuwafuata wananchi kwa ajili ya kuwasikiliza na kutatua kero zao.
Katika Mkutano huo wataalamu mbalimbali wa Ardhi wakiwemo Kamishna msaidizi Mkoa na timu yake, kwa kushirikiana na wataalamu wa Ardhi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa wametoa elimu kuhusu sifa na mchakato mzima wa kumiliki Ardhi.
Akizungumza na Wananchi hao Kamishna msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma Bwana Thadei Kabonge, amesema ili eneo liweze kusajiliwa na kupatiwa hati ni lazima liwe kwenye mpango wa upimaji ardhi na lisiwe na mgogoro.
Ameongeza kuwa, Ili kurahisisha zoezi la upimaji na utoaji wa hati za viwanja, ni muhimu wananchi kuepuka migogoro ya ardhi, huku akisisitiza suala la Wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya ardhi kwa kutokufanya kitu chochote kwenye ardhi kinachoweza kuwa kero kwa wengine.
Kwa mujibu wa Bwana Kabonge, Umiliki wa Ardhi unaanza pale mwananchi anapomiliki hati ya ardhi husika na si vinginevyo na kwamba eneo la Kibaigwa tayari lipo kwenye mpango wa upimaji ardhi na hivyo hairuhusiwi kujenga pasipo kuwa na kibali cha ujenzi.
Naye Msajili wa Hati Mkoa, bwana Geofrey Mavya, amewaeleza wananchi wa Mji mdogo wa Kibaigwa faida mbalimbali za kuwa na hati miliki ya ardhi ambazo ni pamoja na kutumika kama dhamana ya mali isiyohamishika kwenye baadhi ya mahitaji ya kisheria.
Akitoa Elimu kuhusu majukumu ya ofisi ya Msajili wa Hati bwana Geofrey Mavya amesema ofisi yake ndiyo yenye dhamana ya kusajili nyaraka zote za kisheria.
Nao wananchi mbalimbali waliohudhuria Mkutano huo walipata fursa ya kuwasilisha kero zao kwa njia ya maswali ambayo yalijibiwa na wataalamu husika papo hapo.
Miongoni mwa kero zilizoshughulikiwa ni pamoja na utoaji wa hati kwa wananchi wenye nyaraka hai za viwanja vilivyopimwa, sambamba na uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa (NIDA), zoezi ambalo lilichangamkiwa na Idadi kubwa ya wananchi.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Vitambulisho vya Taifa Wilaya ya Kongwa hadi kufika Tarehe 8 Novemba 2022, zaidi ya namba za NIDA 12,576 zimetolewa kwa wakazi wa Mji mdogo wa Kibaigwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.