Wananchi wa Kijiji cha Njoge kilichopo Kata ya Njoge wamelalamikia uongozi wa Serikali ya Kijiji hicho kwa kuwa na tabia ya kufanya maamuzi bila makubaliano ya Pamoja.
Wananchi hao wameeleza hayo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Mayeka Simon Mayeka alipotembelea kijijini hapo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi kutatua mgogoro wa ardhi Kati ya kijiji cha Njoge na Kijiji cha Lenjulu kilichopo Kata ya Lenjulu.
Wananchi hao wamesema viongozi wapya walioingia madarakani hivi karibuni hawajawahi kufanya mkutano wowote na wananchi na badala yake wamefanya mabadiliko kadhaa bila kuwashirikisha ikiwemo swala la kupandisha bei ya maji tiririka kutoka shilingi 20 hadi shilingi 50 kwa ndoo moja yenye ujazo wa lita 20.
Akijibu hoja hiyo kwa niaba ya meneja wa Ruwasa Wilaya ya Kongwa Bi Provina singenda amesema kuwa suala la bei za Maji kwa sasa zinapangwa na wizara ya Maji ambapo ndoo moja ni shilingi 20 kwa Maji tiririka, shilingi 40 kwa Maji ya visima na shilingi 1,000 kwa Unit moja ya Maji ya majumbani ambapo ni sawa na ndoo 50.
Aidha Bi Singenda ameongeza kuwa katika bajeti ya Mwaka wa fedha 2024/2025 kijiji hicho kitajengewa tenki la Maji la lita 100, 000 hivyo wananchi hao waendelee kuwa na subira maana swala hilo liko katika utatuzi na karibuni changamoto ya upungufu wa Maji iliyopo kwa sasa itapatiwa utatuzi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Njoge Bwana Hassan Kalambo amekiri kuwepo kwa malalamiko hayo na ameomba radhi kwa wananchi na kuahidi kuanza kuweka vikao vya mara kwa mara kuzungumzia maswala mbalimbali ya Kijiji na kufikia maamuzi kwa pamoja.
Kwa upande wake mhe. Mayeka amesema kuwa suala la wenyeviti na watendaji wa Vijiji kutokuitisha mikutano kusoma taarifa za mapato na matumizi na kutowashirikisha wananchi juu ya kila kinachojiri ndani ya kijiji ni kosa kisheria n ani Kwenda kinyume na viapo vyao walivyoapa na kutamka kipindi wanaanza kazi na kuwaasa wabadilike.
Baada ya kukaa vikao vya ndani na viongozi wa pande zote mbili za Vijiji vya Njoge na Lenjulu pamoja na mikutano ya hadhara ya wananchi wa Vijiji hivyo, suala la mgogoro wa mpaka wa Vijiji hivyo haukuafikiwa, hivyo viongozi wamekubaliana kupanga siku kufika katika eneo linalogombaniwa kuona mpaka huo na kutoa muafaka ili kumaliza mgogoro huo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.