Wananchi katika Kijiji Cha Chamae kilichopo Kata ya Hogoro wilayani Kongwa wameiomba Serikali kubomoa tenki la maji ambalo limechakaa sana linaloweza kuleta athari kwa jamii.
Wananchi hao wameeleza hayo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Mayeka Simon Mayeka alipotembelea Kata ya Hogoro ili kuongea na wananchi kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika Maeneo yao ambapo wameeleza kuwa baada ya tenki hilo kuchakaa Kwa Sasa wanatumia tenki la plastiki lenye ujazo wa lita 12,000.
Kupitia changamoto hiyo Mh Mayeka ameagiza wakala wa maji vijijini (RUWASA) wilaya kuhakikisha wanachukua hatua za haraka kuja kubomoa tenki hilo kitaalam bila kuleta madhara kwa wananchi na kuwataka Mamlaka za maji na barabara kuitisha mkutano ya hadhara kutambulisha miradi kabla haijaingia vijijini.
Aidha Mh Mayeka amewataka wananchi kulinda miundombinu ya Serikali kwani inaletwa kwaajili ya kuwasaidia wenyewe aidha watunze maeneo yote ya hifadhi ya vijiji ili iwasaidie pale inapotokea miradi mbalimbali ya maendeleo.
Pia Mh Mayeka amesema kuwa suala la mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Mkutani kilichopo wilaya ya Kongwa na kijiji cha mlimwa kilichopo wilaya ya Chamwino kuwa atakaa na mkuu wa wilaya ya Chamwino kupitia mpaka uliopo kuona namna ya kulimaliza mgogoro huo na pia mgogoro wa kugombania shamba kati ya Kijiji cha Nyerere na timu ya ardhi itakuja kupitia mpaka na mwenye shamba atapewa matumizi ya ardhi yake.
Akijibu baadhi ya changamoto mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt Omary Nkullo amesema suala la ukosefu wa kituo cha afya katika Kata ya Hogoro hilo linajulikana kwani wilaya ina Kata 22 lakini Kata zenye vituo vya afya ni 10 tu hivyo wameanza kutoa kipaumbele kwa Kata za pembezoni na muda utakapofika Kata ya Hogoro itapatiwa kituo cha afya hivyo waandae maeneo na kuanza hatua za awali za ujenzi.
Dkt Nkullo ameongeza kuwa ukosefu wa walimu wa shule za msingi na Sekondari wanalipokea na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kibali cha kuajili wafanyakazi wa sekta ya elimu watapangwa katika Halmashauri hivyo basi watatoa kipaumbele kwa shule za Kata ya Hogoro kwani kumeonekana na upungufu mkubwa wa walimu na wahudumu wa afya 100 watakapokuja wataongezewa ili kurahisisha huduma ya afya.
Aidha Dkt Nkullo ametolea ufafanuzi upungufu wa vyumba vya madarasa wananchi waendelee kuweka maeneo na kuanza ujenzi wa vyumba vya madarasa na Halmashauri itakuja kusaidia Kwa hatua za umaliziaji aidha visima vya umwagiliaji 150 vilivyopangwa kuja Wilaya ya Kongwa vitakapoletwa watapatiwa kama walivyoahidiwa hapo awali.
Akitolea ufafanuzi suala la wananchi kulima katika njia za kupitishia mifugo mwanasheria wa Halmashauri bwana Fadhili Msomi Mboyi amesema kuwa ni kosa kisheria mtu kufunga njia ambayo watu wanatumia kwenda kupata huduma sehemu fulani kwahiyo wananchi wanaolima hadi kwenye njia ya kupitishia mifugo wanavunja sheria waache mara moja au wachukuliwe hatua za kisheria.
Akiongea kwa niaba ya meneja wa wakala wa barabara za vijijini na mijini (TARURA) wilaya ya Kongwa mhandisi Mashaka Ngeleja amesema barabara ya kutoka mkutani kwenda matanga na kutoka Hogoro kwenda Chigwingwili tayari wakandarasi wamepatikana wapo eneo la kazi kwahiyo changamoto ya barabara itatatuliwa, pia barabara ya Kongwa kwenda Arusha wananchi walio pembezoni wasifanye mwendelezo wa ujenzi wa makazi mita 30 upande wa kulia na kushoto kwani tayari ipo kwenye mpango wa ilani ya chama cha Mapinduzi CCM wakati wowote ujenzi utaanza.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.