Na Stephen Jackson, Kongwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amewataka wananchi kushirikiana na Serikali kulinda miundombinu ya miradi ya Kuhimili mabadiliko ya Tabianchi inayotekelezwa na Shirika la FECE (Foundation for Energy Climate and Change) Kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Dkt. Jafo amebainisha hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kata za Ugogoni na Sejeli katika Kijiji cha Machenje wakati akizindua Mradi wa Josho la kuogeshea mifugo April 13, 2024 .
Akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Afisa Mifugo Wilaya ya Kongwa Bwn. Msafiri Mkunda amesema mradi huo wa Josho lenye ujazo wa Lita elfu kumi na mbili umekamilika na shughuli za uogeshaji zinaendelea kwa asilimia tisini na wananchi kupitia kamati ya uendeshaji, wamejiwekea utaratibu maalum wa kuendesha Josho hilo kuchangia shilingi mia moja Kwa ngombe na shilingi hamsini kwa mbuzi na kondoo, fedha zinazowezesha ununuzi wa dawa.
Katika kikao baina yake na Kamati ya ulinzi na Usalama, Wakuu wa Divisheni na Vitengo na Viongozi wa shirika la FECE, amesisitiza usimamizi mzuri wa miradi Ili Serikali iweze kufikia malengo ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
Akizindua Josho la kuogeshea mifugo katika Kijiji cha Machenje, Waziri Jafo amefurahishwa na utekelezaji wa mradi huo, na hivyo ametoa maelekezo kwa wasimamizi wa mradi kukamilisha uwekaji wa miundombinu ya Maji Ili kufanikisha lengo la mradi huo.
Akizungumza mbele ya Wanakijiji wa Kijiji cha Machenje, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel ameahidi kushirikiana na Viongozi wa Halmashauri kuhakikisha miradi inasimamiwa vizuri.
Naye Diwani wa Kata ya Ugogoni Mhe. Elizabeth Lenjima ameishukuru Serikali kwa kujenga mradi huo, akiamini kwamba wananchi wa Kata yake sasa watakula nyama salama inayotokana na mifugo salama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Machenje bwana Bwn. Hamis Jonasi Lechipya ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Josho hilo kwani limeanza kuwaletea manufaa baada ya Wananchi kukosa huduma ya kuogesha mifugo yao.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.