Na Stephen Jackson, Kongwa.
Meneja wa RUWASA (Wakala wa maji vijiji na Usafi wa mazingira) Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma mhandisi Kaitaba Rugakingira, ameonya tabia ya uharibifu wa miundombinu ya maji unaofanywa na watu wasio waaminifu katika maeneo mbalimbali.
Rai hiyo imetolewa tarehe 27 Septemba, 2022 wakati akihitimisha semina ya siku mbili kwa wajumbe wa vyombo vya watumia maji ngazi ya jamii, iliyofanyika ukumbi wa VETA Kongwa ikihusisha kata mbili za Ugogoni na Mtanana zinazonufaika na mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi, unaotekelezwa na Shirika la "Foundation for Energy, Climate and Environment" (FECE)
Mhandisi Rugakingira ameeleza kuwa uharibifu wa miundombinu hupelekea matengenezo ya mara kwa mara, hivyo amewaagiza wajumbe wa kamati hizo kuhakukisha wanailinda miundombinu ya maji katika maeneo yao.
Aidha ameongeza kuwa yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria Ikiwa ni pamoja na kulipa faini kati ya shilingi milioni Moja hadi milioni tano.
Mhandisi Rugakingira, amezishauri kamati za usimamizi wa maji kufunga mita maalumu (bulk meter) kwenye matenki ya maji Ili kubaini kiasi halisi cha maji kinachosambazwa kwa watumiaji.
Naye mtaalamu wa elimu ya jinsia na mkufunzi wa semina hiyo ndugu Emmanuel Mroto kutoka kituo cha jinsia SUA, ameeleza kuwa kwa muda mrefu mahitaji ya wanawake yamekuwa hayapewi kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya jamii hivyo Kuna Kila sababu ya kuijengea uwezo jamii.
Akichangia hoja katika semina hiyo, Samson Lazaro Daudi mkazi Kata ya Mtanana, amewataka viongozi wa vijiji kutekeleza majukumu yao kwa weledi Ili kuzuia migogoro ya ardhi na uharibifu wa Mazingira vikiwemo vyanzo vya maji.
Kwa upande wake Remmy Malogo Mwenyekiti wa chombo cha watumia maji Kijiji cha Ibwaga pamoja na kukiri kunufaika na semina hiyo, pia ameshauri kuwepo kwa tathmini endelevu ya utendaji kazi Ili kubaini tija ya mafunzo hayo.
Kwa upande wao Mafundi wa miradi ya maji Sospeter Mkoma wa Chigwingwili na Bahath Packshard wa Mtanana "B" wametoa shukurani kwa RUWASA na FECE kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamewajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto kadha wa kadha.
Mafunzo haya ya kuwajengea uwezo wajumbe wa vyombo vya watumia maji, yamewanufaisha washiriki kwa kuwafunulia mbinu na maarifa mapya juu ya usimamizi wa miradi ya maji na utunzaji wa Mazingira.
Katika semina hiyo kamati hizo zimeshauriwa mbinu mbalimbali za kuziba mianya ya upotevu wa maji na mapato ikiwemo kuwaelimisha wananchi, na kuhamasisha matumizi ya mita za kisasa za malipo ya Kabla ya bili za
maji (LUKU), ambapo mteja hulipa huduma ya maji kadiri anavyotumia.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.