Na Stephen Jackson, Kongwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel amewaonya wananchi wanaonunua mahindi yanayouzwa na Serikali kwa bei nafuu kwa lengo la kuyauza Kwa bei ya juu kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato.
Mhe. Mwema amesema hayo wakati wa kikao cha kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichofanyika Ukumbi wa chuo cha VETA Mjini Kongwa tarehe 19 Desemba, 2022.
Kupitia rai hiyo, Mhe. Mwema amesema Serikali haitosita kuwachukulia hatua wananchi wa aina hiyo kwani kufanya hivyo ni kuhujumu uchumi.
Kwa mjibu wa Mkuu wa Divisheni ya kilimo Wilaya ya Kongwa Bwana Jackson Shija, Kamati ya maafa ya Wilaya iliomba jumla ya tani 400 za mahindi kutoka kwa wakala wa hifadhi ya chakula ya Taifa, ili kupunguza mfumuko wa bei ya chakula na jumla ya tani 121.8 zimepokelewa huku tani zipatazo 90 zikiuzwa katika Kipindi kifupi.
Katika mchakato wa uuzaji wa mahindi hayo, kila mwananchi anayehitaji kununua anapaswa kufika katika maghala husika akiwa na barua ya Mtendaji wa Kijiji, na ataruhusiwa kununua kiasi kisichozidi "kilogram" hamsini.
Sambamba na hayo amekemea tabia ya uharibifu wa Mazingira inayofanywa kwenye Maeneo Mbalimbali ikiwemo utupaji taka ovyo hususani katika Barabara kuu ya Dodoma-Morogoro ambapo Msafiri yeyote atakayebainika atatozwa faini ya shilingi laki tatu.
Kikao hicho kimejadili mambo Mbalimbali ikiwemo miradi ya Serikali katika sekta Mbalimbali na kupokea maoni kutoka kwa wajumbe kwa lengo la kuboresha ufanisi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.