Wanawake wametakiwa kuzingatia malezi ya watoto kwa kuwalea watoto wote kwa pamoja bila kubagua. Wanawake pia wamekumbushwa zama za zamani ambapo kulikuwa na msemo wa, ‘mtoto wa mwenzako ni wako.’
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Kiwilaya yaliyofanyika katika Kata ya Mlali Kijiji cha Mlali Iyegu ambapo ameeleza kuwa wazazi kwa kushirikiana na viongozi wa dini watafakari na kufuatilia malezi ya watoto na familia ili kujenga jamii bora yenye maadili.
Aidha Mhe. Mayeka amewasisitiza wanawake kuomba amani kwa familia zao na Taifa zima na kuwataka Wanawake kuvunja ukimya na kujitokeza kwa wingi katika kufuatilia haki zao za masuala ya ndoa na mirathi wakisaidiwa na huduma ya msaada wa kisheria wa mama Samia.
Mhe. Mayeka pia amefafanua suala la usawa wa kijinsia kuwa kitendo cha nchi kuongozwa na Rais mwanamke ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya mkutano wa Beijing kuwawezesha wanawake kushika nafasi nyingi na za juu katika uongozi.
Kwa upande wake Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Kongwa Mhe. Job Ndugai ametilia mkazo suala la malezi kwa watoto wa jinsia zote kwani kwa kipindi cha hivi karibuni nafasi ya mtoto wa kiume imepotea kutokana na wazazi kuegemeza malezi zaidi kwa mtoto wa kike jambo linalopelekea mtoto wa kiume kusahaulika kwa kiasi kikubwa.
Vilevile Mhe. Ndugai amewataka wazazi kuacha kuwachanganya watoto wao na wageni wenye tamaduni tofauti na za kitanzania, kwani dunia kwa sasa imebadilika hivyo ni jukumu la wazazi kuwalinda Watoto wao na tamaduni za nje ambazo sio za kitanzania ili kukuza taifa linalojivunia tamaduni za kiafrika.
Nae katibu wa chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kongwa Bi Joyce Mkaugala amesema wanawake sasa wanaweza kujitegemea kutokana na kujishughulisha katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuongeza pato la familia na Taifa hivyo wanawake waendelee kushikamana na pia kuwajengea kujiamini Watoto kuwa wanawezakufikia malengo yao wanayojiwekea pindi wanapoweka juhudi.
Aidha, akiunga mkono kauli mbiu ya siku ya wanawake inayosema "wanawake na Wasichana 2025, Tuimarishe Haki, usawa na Uwezeshaji" mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhe. White Zuberi ameitaka jamii kuacha kuwafanyisha kazi za ndani watoto wa kike badala yake wawapeleke shule ili wapate fursa ya elimu itakayokuja na kazi nzuri zitakazowapatia kipato kizuri miaka ya mbeleni.
Naye kamanda wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU Wilaya ya Kongwa Bwana Cosmas Shauri amewataka wanawake kuacha tabia ya kuwa na mahitaji ya juu kuliko uwezo wao au uwezo wa wenza wao kwani hali hiyo hupelekea kujiingiza katika vitendo vya rushwa ili kupata kipato cha ziada kukidhi mahitaji hayo makubwa.
Akisoma taarifa ya maendeleo ya Jamii, Afisa maendeleo ya Jamii Bi. Faraja Kasuwi ameeleza kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali zinazowakumba wanawake kama vitendo vya ukatili, uwepo wa mila na desturi kandamizi kama kutoruhusiwa kurithi mali pindi wanapofiwa na wenza wao na kueleza kuwa mikakati imewekwa ili kudhibiti changamoto hizo. Bi Kasuwi ameeleza baadhi ya mikakati hiyo ikiwemo ushiriki wa wanawake katika vikundi na kuibua miradi, kupinga kwa Pamoja na kupaza sauti dhidi ya Mila na desturi kandamizi, kutoa elimu kwa wananchi kuacha Mila potofu zinazomkandamiza mwanamke na mtoto wa kike.
Mbali na hayo kundi la wanawake wajawazito kutoka Kijiji Cha Mlali Iyegu wakiongozwa na Bi Sophia Chomola (26) wamesema kuwa wanaomba Serikali kuboresha huduma za afya upande wa kliniki ya baba, mama na mtoto, ikiwemo huduma bora za kujifungulia na ongezeko la madaktari wa kutosha ambapo ombi hilo limechukuliwa na kufanyiwa kazi kwa Serikali.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.