Kamati ya Lishe wilaya ya Kongwa, Imepiga marufuku walimu kutumia mashamba ya shule kwa manufaa binafsi, na badala yake Imeelekeza mashamba hayo yatumike kuzalisha chakula cha wanafunzi.
Agizo hilo limetolewa na Afisa Lishe Wilaya ya Kongwa Bibi. Maria Haule wakati wa kikao cha kamati ya lishe cha kupokea taarifa za utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha robo ya pili.
Bibi Haule amesisitiza pia jamii kutumia chumvi yenye madini joto kama njia ya kujikinga na magonjwa.
Akichangia hoja, CPA. Deodatus Mutalemwa, mkuu wa Kitengo cha Fedha ameshauri suala la kudhibiti usambazaji wa chumvi isiyo na madini joto lifanyike katika ngazi za juu badala ya kuwaachia maafisa lishe na Afya wa Wilaya.
Mjumbe Gisiri Chacha kutoka divisheni ya Elimu, alishauri busara itumike kwenye kutekeleza agizo la kupanda mbegu ya mtama kwenye mashamba yote ya shule, badala yake kwa maeneo yanayoruhusu kustawisha mazao mengine waruhusiwe kupanda ili kuepuka hasara inayoweza kusababishwa na ndege waharibifu kwa zao la mtama.
Naye Mtaalamu wa Kilimo Bi. Amina Mussa licha ya kukiri uwepo wa changamoto ya ndege waharibifu, ameshauri wakulima kutumia njia za asili kukabiliana na ndege pindi wanapo jitokeza huku wakishirikiana na wataalamu wa kilimo kwa hatua zaidi.
Wilaya ya Kongwa inatekeleza mkakati wa kila shule kulima mazao ya chakula ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa chakula shuleni linalochangia ufaulu hafifu wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Kwa mujibu wa Haule, takribani shilingi milioni 21 kati ya 31 zilizotengwa kwenye bajeti ya lishe kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 sawa na asilimia 68% zimetumika
Kwa mujibu wa wajumbe wa kamati, shule nyingi za msingi na Sekondari wilayani Kongwa, zinaendesha shughuli za kilimo katika msimu huu, licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo hofu ya ndege waharibifu wa mazao.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.