Waganga wafawidhi wa Vituo vya Afya, na Waratibu Elimu Kata kutoka kata 22 zilizo katika Wilaya ya Kongwa kupitia Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) nchini wamepata mafunzo ya siku mbili juu ya namna ya kutumia mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha unaojulikana kwa Kiingereza kama “Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS)”.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma na kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi katika hesabu za mapato na matumizi ya Halmashauri.
Aidha, kuunda kwa mfumo huo kutasaidia kuhakikisha fedha za ruzuku zinasimamiwa vizuri na taarifa za matumizi yake zinatolewa kwa usahihi tofauti na ilivyokuwa mwanzo. Mfumo huu (FFARS) utawapatia watoa huduma mfumo sanifu uliorahisishwa ambao utawawezesha kutunza taarifa za fedha zinazotolewa na zilizopo katika vituo vyao. FFARS itaweza kufuatilia matumizi ya fedha hizo katika kufikia malengo ya utoaji huduma na kuhakikisha kuwa yanaendana na sheria za manunuzi na utoaji taarifa.
Taarifa zitazotokana FFARS zitasaidia Serikali kuimarisha Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma na kuongeza uwazi, na hivyo watoa huduma wa afya kuwa na wajibu kwa jamii wanayoihudumia.
Mfumo huo wa FFARS unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI); Wizara ya Fedha na Mipango; Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi; na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pamoja na USAID.
Mafunzo hayo yanafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri, ambapo Maafisa (Waratibu) Elimu Kata 22 na Waganga Wafawidhi 4 toka Vituo vya Afya wameshiriki. Mafunzo hayo pia, yanatarajiwa kuwanufaisha waganga wa Zahanati zote 45, wakuu wa shule za msingi 105 na shule za sekondari 31 za Serikali zilizopo Wilayani Kongwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.