Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Wanafunzi wa shule za Msingi wanaoshiriki michezo ya UMITASHUMITA wametakiwa kudumisha nidhamu na kuzingatia masomo ya darasani.
Ujumbe huo umetolewa na viongozi wa Wilaya ya Kongwa muda mfupi kabla ya wanafunzi 108 kuvunja Kambi ya michezo ya Wilaya iliyokuwa katika shule ya msingi Viganga ili kuelekea Shule ya Sekondari Dodoma Kwa mashindano ngazi ya Mkoa.
Akizungumza katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, aliwataka wanafunzi hao kudumisha nidhamu na kushiriki mashindano ipasavyo ili waweze kurejea na ushindi. "Mkienda nsijanjaruke" Alikaririwa Mwema.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo aliwataka wanafunzi kuongeza bidii katika masomo yao ili kuiletea heshima Wilaya hiyo.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Bi. Margareth Temu akiwa Kambi hapo alisisitiza nidhamu kwa wanafunzi hao akiamini kuwa ndio Msingi wa ushindi na akawataka kushiriki hadi mwisho.
Kwa upande wake Mratibu wa Michezo hiyo ngazi ya Wilaya Mwl. Obedi Ngole alisema wanafunzi hao watashiriki michezo mbalimbali ya viwanjani na fani za ndani hususani kwaya na Ngoma za Asili.
Mlezi wa Wanafunzi hao Mwalimu Sarah Luhende, amethibitisha kuwa wanafunzi hao wapo vizuri katika suala la nidhamu na ameahidi kurudi na ushindi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.