Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Kamati za usimamizi wa miradi ya BOOST, zimetakiwa kukuza uwazi na uwajibikaji ili kufanikisha malengo ya miradi hiyo.
Hayo yameelezwa na viongozi mbalimbali wilayani Kongwa katika kikao maalumu kilichoitishwa na Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa kwa lengo la kujadili mikakati mbalimbali ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo kupitia mradi wa BOOST.
Mhe. Mwema alisisitiza kamati kuzingatia taratibu na kanuni katika kuajiri mafundi ili kupunguza malalmiko. Sanjali na hayo ameziagiza kamati kuweka kipaumbele kwa mafundi waliopo katika maeneo husika ili kuongeza mzunguko wa fedha katika maeneo hayo.
Kufuatia hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo amewataka wasimamizi wa mradi kuwashirikisha wananchi kikamilifu kwa njia ya uwazi ili kuwaondoa mashaka.
Akizungumza katika kikao hicho, Afisa elimu ya Awali na Msingi Bi. Margareth Temu alisema mradi wa BOOST utajenga shule mpya mbili, madarasa 26, madarasa mawili ya awali, darasa moja la elimu maalum na matundu 18 ya vyoo.
Naye Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Kongwa Bwana Cosmas Shauri alishauri michakato yote inayohusiana na mradi kuanza mapema ili kuharakisha mchakato wa utekelezaji.
Akitoa Rai kwa wajumbe, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kongwa Mwalimu Abdi Mussa Matari, aliwaasa wasimamizi wa mradi kuacha ubinafsi badala yake wajielekeze kwenye uwazi na ushirikishaji.
Akichangia agenda, Kaimu katibu Tawala wilaya ya Kongwa Bi. Mamndolwa Gembe alizielekeza kamati za usimamizi miradi kuzingatia usalama wa wafanyakazi kwa kuwaepusha na mazingira hatarishi.
Akitoa shukrani zake, Diwani wa Kata ya Chiwe Mhe. Omary Mlimaoga alishauri kuwa kwenye maeneo yenye ujenzi mkubwa ni vema wakaajiriwa mafundi wengi ili kuharakisha ukamilishaji wa mradi.
Wakielezea manufaa ya kikao hicho, Mratibu wa Mradi, Bi. Gwantwa Kabunduguru na Mwalimu Sifrasi Nyakupora Afisa Elimu Kata ya Chamkoroma, wamesema kikao hicho kimewaleta pamoja wadau wote wanaohusika na utekelezaji miradi hivyo itawezesha kufuatwa kwa taratibu mbalimbali.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.