Na Mwandishi Wetu, Kongwa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Fatuma Mganga amewataka wasimamizi wa Miradi Mbalimbali ya ujenzi kusimamia kikamilifu fedha zilizotolewa na Serikali ili kukamilisha miradi hiyo.
Katika Maelekezo yake, amewataka wasimamizi wote wa miradi kuhakikisha vifaa na mali ghafi za ujenzi vinanunuliwa kwa kuzingatia bei elekezi na vinatumiwa kwa umakini Ili kuwezesha miradi kukamilika.
Dkt. Mganga amesema hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi tarehe 21 Novemba, 2022.
Akirejea ushauri wa Kitaalamu, Dkt. Mganga amezielekeza kamati za ujenzi kutumia "wall put" badala ya "gypsum powder" kumalizia kuta za Majengo, Ili kupunguza gharama huku ubora wa Majengo ukizingatiwa kwa kuweka marumaru badala ya sakafu ya kawaida, hasa kwa Vyumba vya Madarasa.
Nao wasimamizi wa Miradi Mbalimbali iliyokaguliwa wameeleza changamoto Mbalimbali zinazojitokeza kwenye utekelezaji wa Miradi, ikiwa ni pamoja na mfumuko wa bei ya vifaa vya ujenzi, na baadhi ya Maeneo jamii kuwa na ushirikiano hafifu katika kujitolea nguvu kazi na michango ya hali na mali.
Aidha amekemea vikali Matumizi mabaya ya fedha za Serikali na kwamba Serikali haitosita kuchukua hatua.
Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na Shule ya Sekondari White Zuberi, Shule ya Sekondari wasichana Ibwaga, Shule ya Sekondari Sagara, Zahanati ya Kijiji cha Suguta Kata ya Iduo, Shule ya Sekondari Ihanda (Mlali), Kituo cha Afya Pandambili, Zahanati ya Lenjulu na Shule ya Sekondari Dr. Nkullo.
Timu hiyo ya Ukaguzi wa miradi iliyoongozwa na Katibu Tawala Mkoa aliyeambatana na wataalamu Mbalimbali wakiwemo Afisa Mipango na Mhandisi wa Mkoa, Imetoa Maelekezo Kwa wasimamizi wa miradi Mbalimbali ya ujenzi kuhakikisha inakamilika ifikapo tarehe 8 Desemba, 2022.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.