Kongwa, Dodoma.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametambulisha mradi wa utafiti wa mnyoo tegu wa nguruwe ujulikanao kwa jina la ‘neurosolve project’ katika kikao na wajumbe wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa. Baada ya kuwatambulisha wajumbe wa Halmashauri, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa dkt. Omary Nkullo akamkaribisha Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. White Zuberi Mwanzalila ambaye alitumia wasaa huo kufungua kikao rasmi.
Akitoa elimu kwa niaba ya watafiti waliohudhuria katika kikao hicho, Dkt. Ernatus Mkupasi, Mtafiti na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ameelimisha wajumbe wa Halmashauri kwa kuelezea mzunguko mzima wa kusambaa kwa mnyoo tegu kati ya binadamu na nguruwe.
Dr. Ernatus Mkupasi, Mtafiti na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) akitoa elimu kwa wajumbe wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Dkt Ernatus Mkupasi ameeleza mzunguko wa mnyoo tegu kutoka kwa binadamu Kwenda kwa nguruwe na kutoka kwa nguruwe Kwenda kwa binadamu na ameanza kwa kueleza kuwa mnyoo tegu akiwa tumboni kwa binadamu,huishi katika utumbo mwembamba na anaweza kukuwa kwa urefu wa mita sita mpaka kumi, mnyoo huyo akishakomaa huwa anaachia pingili zilizopo kwenye sehemu ya mkia wake, watafiti wamebaini kuwa pingili moja hubeba mayai takribani elfu Hamsini. Pingili hizo hutoka katika utumbo wa binadamu kwa njia ya haja kubwa. Tabia hatarishi za binadamu ikiwemo kujisaidia katika vyanzo vya maji ama maeneo yasiyo rasmi kutumika kama vyoo husababisha kusambaa kwa mayai haya kwenda kwa nguruwe kwa njia mbalimbali. Mfano nguruwe akitumia maji yenye mayai ya mnyoo tegu ama nguruwe akilishwa chakula chenye mayai ya mnyoo huyo. Mayai yaliyoingia katika mwili wa nguruwe huanguliwa na kusambaa sehemu mbalimbali ya mwili wa nguruwe. Nguruwe mwenye mnyoo tegu husambaza mnyoo huo kwa binadamu endapo nyama yake yenye mnyoo tegu italiwa na binadamu.
Mchoro wa usambazwaji wa mayai ya mnyoo Tegu kati ya binadamu na nguruwe.
Mtafiti ameeleza kuwa binadamu mwenye mnyoo Tegu anaweza kusambaza mayai ya mnyoo huyo kwa binadamu mwingine endapo hatazingatia usafi wa kina baada ya kutumia choo na kushikana mikono na binadamu mwingine ambaye kwa namna moja ama nyingine atameza mayai hayo kwa kula chakula bila kusafisha mikono yake. Pia unywaji wa maji yasiyo safi na salama yenye mayai ya mnyoo tegu ni njia mojawapo ya binadamu kumeza mayai ya mnyoo huyo na endapo mayai hayo yataingia mwilini mwa binadamu basi yataanguliwa na ukuwaji wa mnyoo tegu utaendelea katika mwili wa binadamu.
Aidha Dkt Ernatus Mkupasi ameainisha changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kumpata binadamu pindi atakapopata mnyoo wa aina hii na kueleza kuwa binadamu akipata mnyoo Tegu na kukaa kwenye mfumo wa fahamu basi anawezapata changamoto mbalimbali ikiwemo Kupoteza kumbukumbu, Maumivu ya kichwa yasiyoisha,Changamoto za Kifafa, Kupooza na matatizo mengine ya afya ya akili ikiwemo kichaa.
Changamoto nyingine ambazo binadamu anawezakukumbana nazo ni changamoto za kiuchumi ambazo zitaletwa na gharama za matibabu pindi binadamu atakapogundulika kuwa na mnyoo Tegu, lakini pia uharibifu wa nyama na mifugo ambayo imeathiriwa na mnyoo tegu sababu nyama hiyo inakuwa sio salama kutumika tena kwa binadamu.
Akiongea wakati wa kufunga kikao, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhe. White Zuberi ameshukuru watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa elimu iliyotolewa na kuhimiza mchakato huu wa elimu kupitia wataalamu na wajumbe mbalimbali wa Halmashauri uwafikie wananchi ili wapate ufahamu wa changamoto hii ya mnyoo Tegu.
Washiriki katika kikao cha uzinduzi wa Mradi wa mnyoo Tegu wa nguruwe (neurosolve project) wakiwa katika picha ya pamoja.
Uzinduzi wa mradi huu ni muendelezo wa jitihada za dhati zinazofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kushirikiana na serikali Pamoja na vyuo vingine vilivyopo ndani na nje ya nchi, pamoja na wadau wengine wa afya ikiwemo Umoja wa Ulaya ili kutokomeza changamoto hii ya mnyoo Tegu wa nguruwe. Mradi huu pia unalenga kuendelea kutoa elimu endelevu juu ya changamoto hii ambapo elimu hii itagusa maeneo mbalimbali ikiwemo mazingira kwa kuhamasisha usafi wa mazingira na matumizi ya vyoo kwa baadhi ya watu wasiotumia vyoo, lakini pia maeneo mengine kama afya ya mifugo ikihusisha ukaguzi wa nyama kabla haijamfikia mlaji.
Imeandaliwa na;
MASHA E. MBONEA
K/MKUU KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI WILAYA YA KONGWA.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.