Na Stephen Jackson, Kongwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, amewataka Wakazi wa Wilaya ya Kongwa na Watanzania kwa ujumla kutambua na kuthamini historia ya Eneo hilo ambalo lilitumika katika harakati za Ukombozi wa nchi za Kusini Mwa Afrika.
Mhe. Emmanuel alisema hayo wakati akiwa mbioni kuhitimisha ziara ya Mabalozi kutoka nchi tano (5) za Kusini Mwa Afrika hapa nchini Tarehe 02/04/2021.
Aidha Mhe. Mwema ameongeza kuwa, endapo wananchi watathamini historia ya harakati za wapigania Uhuru katika eneo hilo la Kongwa, kitendo hicho kitayapa nguvu Mataifa mengine pia.
"Tunaona Ni heshima kubwa ya kuwa sehemu ya historia ya Nchi za Kusini Mwa Afrika na tungetamani mataifa yote hayo yaweze kutambua hili" Alisema Mhe. Emmanuel.
Akizungumza katika kikao maalumu kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Kongwa Balozi wa Namibia hapa nchini, Mhe. Lebbius Tangeni Tobias, alisema, Kongwa ni sehemu ya pekee kwa kuwa Viongozi wengi waliopigania Uhuru wa Nchi za Kusini Mwa Afrika waliweza kuishi, huku wengine wakipoteza Maisha katika eneo hili.
Naye Balozi wa Msumbiji hapa nchini Mhe. Ricardo Mtumbuida alieleza kuwa Lengo la ziara ya timu hiyo ya Mabalozi ni kujionea halihalisi ya Miundombinu ya kambi ya Wapigania uhuru ili waweze kushirikiana na serikali ya Tanzania hususani Wilaya ya Kongwa kufanya ukarabati wa Majengo kambini hapo kwa Lengo la kutunza historia ya Eneo hilo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Balozi Mtumbuida, ameongeza kuwa Eneo la Kongwa ni miongoni Mwa Maeneo muhimu ya Ukombozi wa Nchi za Kusini Mwa Afrika kupitia hamasa au jitihada za Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere aliyeamini kuwa Tanzania haiwezi kuwa huru mpaka hapo Afrika yote itakapokuwa huru.
Katika ziara hiyo, Mabalozi na Viongozi mbalimbali walipanda miti ya kumbukumbu na kutembelea Maeneo mbalimbali ya kihistoria.
Mabalozi wengine waliokuwepo kwenye ziara hiyo ni Balozi wa Angola Bwana.Sandro De Oliveira, Balozi wa Zimbabwe Lt. Gen. Anselem Senyatwe na Bi. Stella V. Dhlomo kutoka Afrika ya Kusini aliyeambatana na Kanali Bongani Majola.
Kambi ya Wapigania uhuru wa Nchi za Kusini Mwa Afrika iliyopo Wilayani Kongwa, inahusisha Mataifa ya Angola, Msumbiji, Zimbabwe, Afrika ya Kusini, na Namibia.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.