Na Stephen Jackson, Kongwa.
Watendaji vijiji wanaojitolea katika maeneo mbalimbali wilayani Kongwa, wametakiwa kudumisha uzalendo licha ya kukosa nafasi za ajira za kudumu kupitia zoezi la usaili lililohitimishwa Jumapili ya tarehe 4, Septemba 2022.
Salamu hizo zimetolewa na wajumbe mbalimbali wa kikao Cha kamati ya fedha Wilaya ya Kongwa kilichoketi Septemba 5, 2022 chini ya Mwenyekiti wake Mhe. White Zuberi Mwanzalila.
Mhe. White Zuberi Mwanzalila ameieleza kamati kuwa zoezi hilo limekwenda vizuri Kwa kusimamiwa kikamilifu kwa mujibu wa Sheria, taratibu na kanuni ambapo bodi ya Ajira, sekretarieti ya Ajira pamoja na Idara ya utumishi na Utawala walihakikisha haki inatendeka Ili kupata waajiriwa wenye sifa.
Akichangia hoja kwenye taarifa ya Idara ya utumishi na Utawala Diwani wa Kata ya Iduo Mhe. Valentino Seng'unda ameeleza kuwa kutokana na watendaji wa vijiji wa kujitolea kukosa nafasi za ajira za kudumu, ipo haja ya kufanyika vikao rasmi vya makabidhiano kwenye Ofisi zilizo kaimishwa ili kunusuru usalama wa nyaraka kutokana na hisia hasi kwa baadhi ya watendaji waliokosa nafasi za ajira.
"Kwa hasira yao ya kukosa nafasi ya kuwa Watumishi wa Serikali, kutokana na nafasi walizozikosa yawezekana kuna taarifa nyingi zitapotea kwenye eneo lile husika. Sasa ninachoomba kwa kuwa Idara ya utumishi kwa kuwa imeshapata wale wanaotakiwa kuwa na nafasi za utendaji kamili iwe na vikao rasmi vya makabidhiano" Alieleza Mhe. Seng'unda.
Akijibu hoja hiyo, Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi ndugu Fortunatus Mabula amewataka Watumishi hao wa kujitolea kutokata tamaa kwani suala la kukosa ajira hizo siyo mwisho wa maisha na hivyo ametoa wito Maalumu Kwa watendaji hao kufika ofisini kwa ajili ya majadiliano.
"Nimewaomba waje ofisini kwangu waje tujadiliane, wasifikiri ndiyo mwisho wa maisha". Alinukuliwa Ndugu Mabula.
Aidha katika mchakato wa usaili waombaji wa nafasi hizo walipongeza mchakato mzima wa usaili kwa kuzingatia Misingi ya haki na utu.
Kupitia usaili huo jumla ya nafasi 34 za Watendaji wa Vijiji Daraja la III zimejazwa ambapo pindi Watumishi hao wapya watakapo ripoti na kupangiwa vituo vya kazi, hatua hiyo itasitisha mikataba ya watendaji wa kujitolea.
Kikao hicho cha kisheria cha kamati ya Fedha kiliketi kupokea na kujadili taarifa mbalimbali za fedha.
Mhe. White Zuberi Mwanzalila- Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Dkt. Omary Nkullo - Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Mhe. Valentino Seng'unda - Diwani wa Kata ya Iduo
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.