Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel amesema Serikali itawapatia Watendaji wote pikipiki ili waweze kufanikisha shughuli za Serikali katika Maeneo yao.
Mhe. Mwema amesema hayo Februari 17, 2023 wakati akikabidhi pikipiki 6 zilizotolewa na Serikali mnamo tarehe 14 Februari 2023, katika mji wa Serikali mtumba zoezi lililozinduliwa na Dkt. Philip Isdory Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha Mhe. Mwema amesema Kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali pikipiki hizo zitahudumiwa mafuta na gharama za matengenezo kupitia utaratibu maalumu.
Wakati huo huo, ameonya matumizi mabaya ya pikipiki hizo ikiwemo kuzitumia kibiashara na matumizi mengine yasiyofaa kwa Mali za umma.
Sanjali na hayo amewaasa Watendaji kulinda pikipiki hizo dhidi ya wizi Ili kuepusha hasara kwa Serikali.
Awali Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Omary A. Nkullo alisema pikipiki zilizotolewa zililenga kutatua changamoto za usafiri Kwa Watendaji wa kata zote Nchini, lakini Wilaya ya Kongwa imepatiwa sita tu ambazo zinaelekezwa kwenye kata za pembezoni ambazo ni Chitego, Makawa, Njoge, Lenjulu, Chamkoroma, na Ng'humbi.
Wakizungumza baada ya makabidhiano ya pikipiki hizo, Baadhi ya Watendaji hao wameishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio chao hivyo wameiomba Serikali kutupia jicho kwenye changamoto nyingine hususani za uchakataji na uwasilishaji wa taarifa kwa njia za kisasa.
Hadija Salehe Kaimu Mtendaji wa kata ya Sejeli amekaliliwa akisema, Kwenye mchakato wa kuwezesha usafiri wa pikipiki, Serikali izingatie masuala ya jinsia kwani pikipiki aina ya Boxer zinasosambazwa siyo rafiki kwa Watendaji wanawake.
Naye Bwana Moses Sheshe Afisa Mtendaji wa Kata ya Makawa, amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwawezesha pikipiki hizo, kwani zitawasaidia kuwafikia wananchi katika maeneo yao Ili kutatua changamoto zinazowakabili.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.