Na Benadertha Mwakilabi, Kongwa
Wazazi wilayani Kongwa wametakiwa kujitokeza kuwaandikisha kwa wingi watoto wenye umri wa kuanza darasa la kwanza bila kuwaficha wenye ulemavu ili nao wapate haki ya kusoma.
Mratibu elimu kata ya Kongwa bwana Joseph Mwanitu ameeleza hayo katika mkutano wa baraza la mamlaka ya mji mdogo Kongwa walipokutana kujadili taarifa za kamati za kudumu kwa kipindi cha robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Aidha Mwanitu amewataka wazazi kuwaandaa watoto waliomaliza elimu ya msingi kuingia kidato cha kwanza kwa kuwapeleka shule kipindi hiki wanaposubiri matokeo kwani ana uhakika zaidi ya asilimia 90 watafaulu vizuri.
Kwa upande wake Diwani kata ya Kongwa Mhe. White Zuberi Mwanzalila ametoa rai kwa viongozi wa Divisheni ya kilimo kuwahamasisha wakulima kufanya maandalizi mapema Ili kukabiliana na hali ya hewa.
Sanjali na hayo amewataka wananchi kuhifadhi chakula kidogo walicho nacho wakati wakijiandaa na msimu mpya wa kilimo Ili kukabiliana na kipindi cha njaa.
Naye mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo Kongwa Ndugu Onesmo Semundi ametaja changamoto walizokutana nazo na kuzitatua katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na utoro wa wanafunzi, vikundi kukopa na kutorejesha kwa wakati, wakulima kugoma kujisajili na wafugaji kugoma kupeleka mifugo katika vituo vya kuvisha hereni za kielekroniki.
Ameeleza kwamba mamlaka ya mji inatarajia kupokea Tsh 100,000,000 kwaajili ya ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa katika shule ya sekondari White Zuberi na kuwataka wenyeviti wa vitongoji kuanza kuchangisha michango ya mfuko wa elimu haraka ili kuongeza fedha za ujenzi huo kwani hazitoshi kuweka madawati.
Katika mwaka wa fedha 2022/2023 mamlaka imeidhinishiwa kutumia Tsh 94,084,820 na katika robo hii ya kwanza mamlaka imepokea Tsh 15,841,731.00 Kati ya fedha hizo Tsh 10,992.383.60 sawa na 11.68 asilimia imetumika kukarabati jengo la wodi ya wanaume katika hospital ya wilaya Kongwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.