Na Stephen Jackson, Kongwa.
Jamii imeaswa kujenga tabia ya kutembelea hifadhi za taifa ili kukuza utalii wa ndani na uchumi wa taifa.
Rai hiyo imetolewa na wajumbe mbalimbali wakati wa ziara ya kiutalii ya watumishi wa Divisheni ya Elimu msingi wilayani Kongwa katika hifadhi ya taifa Tarangire, iliyofanyika kwa lengo la kuwapongeza watumishi wa Divisheni hiyo kufuatia kupanda kwa ufaulu mwaka 2023.
Akizungumza na watumishi hao katika eneo la hifadhi, Afisa Elimu awali na msingi Wilaya ya Kongwa Bi. Margareth Temu alitoa wito kwa viongozi wa mamlaka na taasisi mbalimbali kujenga tabia ya kuwapa motisha watumishi walio chini yao ikiwa ni sehemu ya kuthamini jitihada zao.
Kwa mujibu wa Bi. Temu Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa imepanda kwenye matokeo ya mitihani ya taifa ya darasa la saba kutoka ufaulu wa asilimia 78% hadi 86%
Akizungumza katika kituo cha starehe (pikiniki center) katika hifadhi hiyo, Msimamizi wa maandalizi ziara hiyo Mwalimu Syfras Nyakupora (AEK - Chamkoroma) ameishauri Mamlaka ya hifadhi kuboreha miundombinu ya Barabara ili kuwezesha magari kuipita kirahisi sambamba na kuboreha viwango vya gharama za usafiri ndani ya hifadhi vitakavyowezesha wananchi wa kipato cha chini kutembelea hifadhi.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa hifadhi ya Tarangire Bwana Josephat Jackson - mwongoza utalii alisema, Katika msimu wa Masika baadhi ya wanyama huhama katika hifadhi hiyo kwa sababu za kiusalama.
Miongoni mwa wanyama walioonekana kwa Wingi msimu huu wakati wa ziara ni makundi ya tembo, twiga, swala n.k huku wanyama wala nyama kama vile Simba, chui, nyati vifaru wakiadimika na kuwaacha watalii wakihaha na kuondoka pasipo kuwaona.
Watumishi hao walipokelewa ofisi za hifadhi hiyo Desemba 17 majira ya saa 02:30 usiku na kuendelea na shughuli za utalii katika mbuga hiyo tarehe 18 na kuondoka asubuhi ya tarehe 19 Desemba, 2023.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.