Wito umetolewa kwa wauguzi kuwajibika kwa kuwa na maadili mema, kutoa huduma bora kwa wateja wao na kuhakikisha wanasimamia matumizi sahihi ya vitendea kazi ili kuzuia vitendo vitakavyoharibu tasnia ya uuguzi.
Wito huo umetolewa na Afisa Elimu sekondari Wilaya ya Kongwa Ndugu Sudy Abdul alipomuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kongwa katika maadhimisho ya Siku ya wauguzi Duniani katika viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya Kongwa ambapo amesisitiza wauguzi kuepuka mianya ya upotevu wa mapato pamoja na vifo vya watoto wachanga na akina mama wanaojifungua.
Mgeni rasmi Mwl. Sudy Abdul akitoa nasaha zake kwenye hafla.
Licha ya kuwapongeza wauguzi, Ndg. Sudi Abdul amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa wauguzi katika kutekeleza majukumu ya afya kwani wanatumia muda mwingi kukaa na wagonjwa na amewaasa waendelee kuwa na kauli nzuri na sura zenye tabasamu kwa wagonjwa ili kuiheshimisha kazi yao.
Aidha Mganga Mkuu Wilaya Dkt. Thomas Mchomvu amesema kwamba haiwezekani kuzungumzia sekta ya afya bila kuwataja wauguzi na kwamba sehemu kubwa ya watumishi wa afya ni wauguzi ambao wana jukumu kubwa la kulinda na kuhakikisha afya za wagonjwa ziko vizuri.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Mchomvu akiongea na watumishi wa afya.
Aidha Dkt Mchomvu ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa katika sekta ya afya ambapo mpaka mwaka 2024, Wilaya ya Kongwa ina vituo vya afya tisa vinavyofanya kazi na kutoa huduma za afya ikiwemo Afya ya uzazi na dharura na kueleza kwamba huo ni utekelezaji mzuri wa ilani ya chama tawala kwa wananchi wake.
Nae Muuguzi Mkuu wa Wilaya Ndg. Cleopa katika risala yake amesema dhumuni la kuadhimisha siku ya wauguzi Duniani ni ili kuimarisha afya ya jamii na kulaani na kupinga vikali vitendo vya wauguzi wasio waaminifu na waadilifu katika kazi zao.
Pia Cleopa ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuruhusu wauguzi kujiendeleza kimasomo, jambo linalowaongezwa wigo mpana wa elimu pamoja na taaluma yao. Ndg. Cleopa pia ameishukuru serikali kwa kuendelea kutoa huduma ya afya ya uzazi na mtoto kwa 88% na kutoa huduma za kujifungua kwa 99% hata katika mazingira magumu na yenye changamoto.
Maadhimisho hayo yaliyokuwa na kaulimbiu "Wauguzi nguvu ya mabadiliko Duniani" wauguzi hao walipata nafasi ya kula kiapo cha maadili chini ya sheria ya wauguzi na wakunga ya Mwaka 2010 mbele ya Mwanasheria Renalda Mkangala wa mahakama ya hakimu makazi mamlaka ya mji mdogo Kibaigwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.