Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, amezindua maabara ya kisasa ya masomo yote ya sayansi katika shule ya sekondari Laikala iliyopo katika Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma yenye thamani ya shilingi za kitanzania milioni 60 iliyojengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Mhe. Hamad Masauni amefanya uzinduzi huo leo alipotembelea wilaya ya Kongwa ikiwa ni sehemu yake ya maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hasani kwa mawaziri kutembelea Mikoa yote ya Tanzania kuona mafanikio ya sekta mbalimbali na Serikali ijiridhishe juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utatuzi wa changamoto katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Pichani ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Eng. Hamad Masauni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka S. Mayeka pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kongwa.
Aidha Mhe. Eng. Hamad Masauni ameonyesha kufurahi kwa kushiriki katika uzinduzi wa maabara ya kisasa katika shule ya sekondari Laikala, ambayo itawezesha wanafunzi kuweza kusoma vizuri masomo ya sayansi na kutimiza ndoto zao kwa kufanya vizuri katika masomo hayo. Akiongea na wanafunzi wa shule ya sekondari Laikala Mhe. Hamad Masauni ameeleza kuwa hivi sasa wanafunzi hawana sababu ya kutopenda masomo ya sayansi kwa ukosefu wa vitendea kazi, kwani maabara ya kisasa iliyozinduliwa hivi leo ni suluhisho na ni tegemeo kuwa watatoka wanasayansi wengi wenye ufaulu mkubwa katika shule ya sekondari Laikala.
wanafunzi wa shule ya sekondari Laikala wakiwa katika maabara iliyozinduliwa na Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Akiongea na wananchi katika mkutano wa hadhara baada ya kukaribishwa, Mhe. Eng. Hamad Masauni ameshukuru wananchi kwa mapokezi mazuri na amefurahishwa na vikundi vya ngoma vilivyotoa burudani katika mapokezi yake, pia ametoa pongezi kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa na vyombo vya ulinzi na usalama kwani Kongwa ni shwari na salama.
Mhe. Eng. Hamad Masauni amefikisha salamu za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Laikala A na ameeleza kuwa ziara yake ni maalumu kwa ajili ya kutimiza wajibu alioagizwa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kukagua miradi ya maendeleo ambayo serikali ya awamu ya sita inatenga fedha nyingi kwa ajili ya kukamilishwa kwa miradi hiyo.
Aidha Mhe. Hamad Masauni, amegusia changamoto ya upungufu wa watumishi wa NIDA katika Wilaya ya Kongwa, pamoja na changamoto ya vifaa kwa jeshi la zima moto na upungufu wa walimu, ambapo Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi emeeleza kuwa Wilaya ya Kongwa itaongezewa watumishi wa NIDA ili wananchi wapate huduma kwa haraka na wepesi zaidi. Akijibu kuhusu upungufu wa vifaa vya zima moto, Mhe. Eng. Hamad Masauni ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan inaleta magari zaidi ya mia na Hamsini, boti na vifaa vingine kwa ajili ya jeshi la zima moto na Kongwa itapata vifaa hivyo pia ili kuondoa changamoto ya upungufu uliopo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Eng. Hamad Masauni akihotubia wananchi wa Kijiji cha Laikala A
Licha ya kuahidi vitendea kazi kwa Jeshi la zima moto lakini pia amekiri kuwepo kwa matukio ya ajali za barabarani zinazotokea mara kwa mara katika barabara ya Dodoma - Dar es Salaam kuwa ni kutokana na kukua kwa matumizi ya barabara hiyo na Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi ambapo katika kudhibiti ajali hizo kutakuwa na mfumo wa kufatilia mienendo ya madereva na magari utakaoanza kabla ya kuisha mwaka wa fedha 2024/25.
Mh Masauni ametaja sababu za ajali hizo kuwa ni matatizo ya kibinandamu, ubovu wa magari na kuwa na miundombinu mibovu na isiyokidhi mahitaji na amesema kuwa Serikali itahakikisha inadhibiti uzembe na kuwachukulia hatua madereva wazembe kwa kuweka Usimamizi madhubuti wa utoaji leseni na kufatilia mara kwa mara matengenezo ya magari.
Aidha Waziri wa Mambo ya Ndani, amefafanua kuwa ni vema wananchi kufahamu mafanikio yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita na kwamba mikakati wa Serikali katika kuimarisha ulinzi na usalama ya kuweka askari kuanzia ngazi ya Kata ni kufanya wananchi kuwa karibu nao na kushirikiana nao kuondoa matukio ya uhalifu lakini pia ni ili askari watimize majukumu yao ya kulinda rai ana mali zake bila changamoto yoyote.
Vilevile Mhe. Hamad Masauni amewasihi Wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji wa wapiga kura litakaloanza tarehe 11-10 mwezi wa 10 mwaka huu kwaajili ya kujiandaa kufanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwezi Novemba tarehe 27 na kuwataka wananchi kufanya maamuzi yenye busara ya kuchagua viongozi bora kwa maendeleo yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameomba Waziri apeleke salamu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa asiwe na wasiwasi kwani katika Wilaya ya Kongwa fedha zinasimamiwa ipasavyo ili kuleta maendeleo yenye tija kwa maisha ya wananchi na amekumbushia kuwa sifa kubwa ya wilaya ya Kongwa ni kuongoza katika usimamizi wa miradi kwani mwaka 2023 Ofisi ya Tamisemi ilitoa tuzo kwa Halmashauri za Wilaya zilizofanya vizuri kwenye usimamizi wa miradi na Wilaya ya Kongwa iliongoza kwa kufanya vizuri. Mhe. Rosemary Senyamule ameongeza kuwa fedha zinazoletwa Kwenda kwenye serikali ya Mkoa wa Dodoma zinasimamiwa kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha ilani ya Chama Cha Mapinduzi inatekelezwa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akiongea na wananchi wa Laikala A.
Ameendelea kwa kusema kuwa ujenzi wa maabara hiyo unatekeleza maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuzitaka kila Halmashauri kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa wananchi wa Halmashauri husika hivyo amemtaka Waziri kutambua kuwa fedha zote zinazoletwa zinasimamiwa vizuri kwenye halmashauri ya Kongwa.
Mwenyeji wa ugeni huo, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka ametoa shukrani zake za dhati kwa ujio wa Mhe. Waziri wa Mambo ya ndani na ametilia mkazo ufuatiliaji wa karibu wa changamoto mbalimbali zilizoainishwa katika mkutano wa hadhara ili wananchi waweze kupata huduma nzuri na maendeleo ambayo serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia suluhu Hassan inaendelea kuwapatia.
Ziara hii ya Waziri wa mambo ya ndani ya Nchi, Mhe. Eng. Hamad Masauni, ni muendelezo wa ziara za kikazi za kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika Wilaya za Mkoa wa Dodoma.
Imeandaliwa na,
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wilaya ya Kongwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.