Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo Alhamisi, Oktoba 11, 2018 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa katika mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Kongwa akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani humo, amesema vitendo vya udokozi wa mali ya umma havitavumiliwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, hivyo amewataka watumishi wawe waadilifu na waaminifu wanapotekeleza majukumu yao.
Aidha, amesema Serikali haitamvumilia mtumishi wa umma ambaye si muadilifu; wavivu na wala rushwa hawana nafasi, hivyo ni lazima watumishi wajibike na ambao watashindwa kutekeleza majukumu yao watapa shida kwenye Serikali hii. “Hakuna mchezo kwenye Serikali hii, watumishi wa umma wanapaswa kulitambua hili.”
Pia, Waziri Mkuu amewataka watumishi hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata maelekezo yaliyotolewa kwenye Ilani ya uchaguzi Chama Tawala (CCM) ya 2015 – 2020.
Waziri Mkuu amewataka pia, watumishi hao wahakikishe wanapanga ratiba ya kwenda kuwatembelea wananchi waishio vijijini na kushirikiana nao katika kutatua kero zinazowakabili si kukaa ofisini, amewataka kutenga kati ya siku tatu au nne za wiki.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kila mtumishi kwenye idara yake anapaswa kwenda kwa wananchi, kama ana siku tano za kufanyakazi kwa wiki basi siku tatu azitumie kwenda kwa wananchi kutatua changamoto zao na kama ana siku sita, siku nne azitumike kuwafikia wananchi.
Kabla ya Waziri Mkuu, Mbunge wa Jimbo la Kongwa ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai, ameishukuru Serikali kwa kutatua kero mbalimbali ikiwemo changamoto ya ukosefu wa maji pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mbande hadi Kongwa ambapo aliomba ujenzi huo uendelee hadi Mpwapwa. Aidha, aliiomba serikali kugawa kwa vipande eneo la Ranchi ya Taifa lililopo wilayani hapo kwa wafugaji kwa kuwa limekuwa halitumiki. “Napendekeza wananchi wapewe vitalu kisha wafuge kwa njia ya kisasa kwa kupatiwa mbegu bora. Hii itasadia kuzalisha bidhaa bora za nyama na maziwa pamoja na wananchi kupata ajira.”
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratias Ndejembi ameishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha za kutekeleza miradi mbalimbali wilayani humo, hadi sasa wameshapokea zaidi ya sh. bilioni tatu kwa ajili ya miradi ya maji. Kuhusu upatikanaji wa dawa kwenye wilaya hiyo alisema umefikia zaidi ya asilimia 90 na wananchi wanapata huduma ya matibabu kwa ubora. “Pia Kongwa hakuna njaa. Tumeweza kuhamasisha kilimo cha mtama kwenye vijiji 89 ambapo Mbunge (Ndugai) alitoa sh. milioni saba kwa ajili ya mbegu ambapo sasa tumeweza kufikia ziada ya tani laki mbili.”
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge amesema mafanikio ya Kongwa ni matokeo ya uwepo wa amani na utulivu kwenye eneo hilo. Hata hivyo, alimwomba Waziri Mkuu baada ya Rais kusaini sheria ya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi ni muhimu ikapewa kipaumbele pamoja na miji mingine midogo inayozunguka jiji la Dodoma kupata fedha za kupima maeneo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.