Na Stephen Jackson, Kongwa.
Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Faustine Mkenda (Mb) amemtunuku afisa ugani wa kata ya Nghumbi wilayani Kongwa ndugu Charles Mujule , Zawadi ya seti ya Runinga ikiwa ni utekelezaji wa Ahadi aliyoitoa mwezi Mei mwaka 2021, alipotembelea shamba la mtama lenye ukubwa wa Ekari Moja, lililolimwa kitaalamu kwa hisani ya shirika la chakula Duniani ‘’WFP’’ na kusimamiwa na afisa ugani huyo.
Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa tarehe 17 Agosti, 2021 mchana ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe, Remidius Mwema Emmanuel ambapo Mhe. Waziri alizungumza na maafisa ugani wa Kata mbalimbali za Wilaya pamoja na wakuu wa Idara.
Katika hotuba yake, Mhe. Waziri amewaeleza maafisa ugani kuwa Serikali itawezesha utekelezaji wa majukumu yao kwa kuwapatia vitendea kazi mbalimbali kama vile pikipiki, simu na pembejeo za kilimo ili kuwawezesha kuinua kipato chao ili nao wasaidie kuwainua wakulima.
Ameongeza kuwa, Serikali inatambua jitihada za maafisa ugani katika kufanikisha mikakati ya Wizara ya Kilimo, hivyo itaendelea kuwathamini, kuwaheshimu na kuwalea ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutowapangia shughuli tofauti na taaluma zao.
Kwa upande wake ndugu Mujule amemshukuru mhe. Waziri Prof. Adolf Mkenda kwa kuthamini jitihada zake kiutendaji, na kuwaasa watumishi wa umma kufanya kazi kwa weledi ili kazi wanazozifanya ziwatambulishe.
Akizunguza baada ya kikao hicho, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Wilaya ya Kongwa Ndugu Jackson G. Shija, licha ya kumpongeza bwana Cherles Mujule, pia ameeleza kuwa Wilaya inaendelea na jitihada za kuendeleza mazao ya kimkakati ambayo ni mtama, Korosho, Alizeti, na Zabibu ambapo kwa mwaka 2020/2021 wilaya imezalisha ziada ya tani 117,978 kwa mazao ya nafaka. Na pia kupitia kikundi cha ZOSEM, Jumla ya tani 18 za mbegu bora ya Alizeti aina ya ''Record'' kwa daraja la kuthibitishwa ubora imezalishwa kwa msimu wa 2020/2021.
Ziara hiyo ya waziri wa kilimo, ilisindikizwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka na Mkutano wake kuhudhuriwa Mkuu wa wilaya ya Kongwa na viongozi mbalimbali wa Halmashauri akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. White Zuberi Mwanzalila, Mkuu wa Idara ya Kilimo ndugu Jackson G. Shija, Diwani wa Kata ya Nghumbi, na Wakuu wa Idara.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.