Mwenyekiti wa Kijiji cha Mlanje Bwana Elisha Mpanda Pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Matongoro, Bw. Joab Chida vilivyopo katika Kata ya Matongoro wilayani Kongwa, wamesimamishwa kazi kutokana na tuhuma za kushindwa kuwajibika na kusababisha migogoro ya ardhi.
Hali hiyo imefikiwa baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka kutembelea Kata hiyo ili kutatua mgogoro wa mpaka kwa wananchi wa vijiji vya Matongoro na Mlanje ambapo wananchi hao wamewalalamikia wenyeviti hao kuvuruga alama za mipaka ya vijiji hivyo kwa maslahi yao binafsi.
Kufuatia hali hiyo Mh Mayeka amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kuhakikisha anatumia taratibu za kisheria kuwasimamisha kazi wenyeviti hao na kushirikiana na mwanasheria wa Halmashauri kusimamia zoezi la upatikanaji wa wenyeviti wa muda katika vijiji hivyo mpaka pale Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) itakapokamilisha uchunguzi wa tuhuma hizo.
Wakiongea mbele ya Mkuu wa Wilaya, wananchi wa vijiji hivyo wamesema kuwa wenyeviti hao wamekuwa wakishirikiana kuvuruga mipaka inayogawa vijiji hivyo kwa kuuza maeneo ya mbuga ya malisho kwa wakulima, suala ambalo ni kinyume na utaratibu, pia wameongeza kuwa wamekuwa wakitishiwa Maisha pindi wanapojaribu kuhoji kwa viongozi hao.
Aidha, wajumbe wa Serikali ya Kijiji cha Matongoro wameongeza kuwa Mwenyekiti wa kijiji hicho amekuwa akikwamisha shughuli za Serikali na pia wamedai kuwa amekuwa akiongoza Kijiji Kwa mabavu na kudai kuwa hakuna kiongozi wa juu zaidi yake hivyo wanatakiwa kumsikiliza yeye na si mtu mwingine.
Wameongeza kuwa uuzaji wa maeneo hayo kinyume cha taratibu ni utekelezaji wake wa ahadi zake za kilaghai alizozitoa wakati wa kampeni kuwa akichaguliwa atawapatia wakulima maeneo pamoja na ahadi nyinginezo ikiwemo kuingiza kaya maskini katika mfuko wa Tasaf ambapo mpaka sasa inasemekana ameshachukua kiasi cha shilingi milioni tatu na kuuza eneo la malisho lenye hekari 80 kwa wakulima.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kijiji Cha Matongoro Bi. Rosemary Lubengo amekiri kutowajibika kwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho na kukwamisha utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na utekelezaji wa ilani ya chama cha Mapinduzi kwa maslahi yake binafsi bila kuangalia hali za wananchi ambao alipaswa kuwatumikia.
Nae Afisa ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Bwana Hansi amesema kuwa mipaka iko wazi kwani upimaji wa mipaka ya vijiji vya Matongoro na Mlanje ulifanyika tangu mwaka 2007 na eneo la malisho lilikuwa sehemu ya Kijiji cha Matongoro lakini baada ya Mwenyekiti huyo kuingia madrakani Oktoba mwaka jana akaanza kuuza eneo hilo kwa wakulima na kusema eneo hilo lipo ndani ya Kijiji cha Mlanje na Sio Matongoro hali iliyoibua mgogoro mkubwa kati ya vijiji hivyo vya Mlanje na Matongoro.
Akifunga hotuba yake Mhe. Mayeka amesema kuwa katika suala la migogoro ya ardhi mara kadhaa viongozi wa vijiji wasio waadilifu wamekuwa ni changamoto na kubainisha kuwa eneo la mbuga ni kwaajili ya malisho na sio matumizi mwengine kama kilimo. DC Mayeka pia ametoa rai kwa viongozi wa vijiji kushikamana katika kuyalinda na kusimamia maeneo hayo ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.