Na Stephen Jackson.
Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwa kushirikiana na wadau wengine, ikiwemo NMB Bank Tawi la Kongwa na “Mawia Enterprises”, wametoa msaada kwa watoto wenye ulemavu wanaohudumiwa katika Kituo cha Kulea Watoto Walemavu cha Mlali (Mlali Rehabilitation Centre For Children) kilichopo Wilayani hapa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika.
Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya, Remidius Emmanuel kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Dkt. Suleiman Serera, amekabidhi msaada huo mbele ya uongozi wa Kituo hicho, lengo likiwa ni kuwasaidia watoto hao na pia kuhamasisha jamii kuwajali watoto wenye mahitaji maalumu. Miongoni mwa vitu vilivyotolewa ni pamoja na vyakula, vinywaji na sabuni.
Katika tukio hili, zaidi ya vitu vyenye thamani ya TZS. 600,000/= zimetolewa na kupokelewa na Msimamizi wa kituo hicho Padri Gaudence Aikaruwa.
Kwa upande wake msimamizi huyo ametoa shukrani za dhati kwa taasisi zote zilizojitolea kuwasaidia watoto hao.
Tukio hili la kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika limehitimishwa baada ya kufanyika kwa mikutano katika Kata 11 Wilayani hapa, ikiwa ni kwa lengo la kuhamasisha upatikanaji wa haki mbalimbali za watoto.
Jumla ya watu 2,045 wameshiriki mikutano hiyo, ambapo kati yao watoto ni 1,524 na watu wazima 581. Miongoni mwa wa wadau walioshirikiana na Halmashauri ya Kongwa katika kuandaa mikutano hiyo ni Shirika la Compassion Tanzania, World Vision, Mahakama ya Mwanzo Kongwa, na Dawati la Jinsia-Polisi Kongwa.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika hufanywa na Nchi wananachama wa Umoja wa Afrika tarehe 16 Juni ya kila mwaka ili kuwakumbuka watoto takribani 2,000 waliouawa Soweto, nchini Afrika Kusini na Serikali ya Makaburu.
Kaulimbiu ya siku hii kwa mwaka 2021 ni ‘‘Tutekeleze Agenda 2040 kwa Afrika inayolinda haki za Mtoto’’.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.