Na. Stephen Jackson, KDC
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel amezindua Zoezi la ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa katika Wilaya ya Kongwa Juni 1, 2023.
Katika zoezi hilo Jumla ya wananchi 65,334 kati ya 120,702 waliojiandikisha watapatiwa vitambulisho vyao huku zoezi hilo likitajwa kuwa endelevu.
Kwa mujibu wa taarifa ya (NIDA) iliyowasilishwa na Bwana Said K. Hamad, Afisa Msajili Vitambulisho vya Taifa (W), Jumla ya namba za vitambulisho vya Taifa 120,702 zimezalishwa Wilayani Kongwa na kati yake vitambulisho 100,334 vimekamilika sawa na asilimia 83% tangu kuanza kwa mpango huo.
Hadi kufikia tarehe 1 Juni 2023, Jumla ya wananchi 20,368 waliojiandikisha Wilayani Kongwa wanasubiri kukamilishiwa vitambulisho vyao huku wanufaika wapya wakiendelea kuandikishwa.
Akihutubia wananchi katika uwanja wa Amani Kibaigwa Mjini, Mhe. Mwema ametoa muda wa siku saba kwa watendaji wa mitaa, vijiji na kata kuhakikisha wananchi wote ambao vitambulisho vyao vimekamilika wanapatiwa.
Aidha ametilia mkazo suala la matumizi sahihihi ya vitambulisho hivyo, ikiwa ni njia pekee ya kufanikisha lengo la kitaifa la kuboresha utoaji huduma kwa wananchi wake.
Naye Bi. Balbina Mtui, kaimu Meneja wa udhibiti na usambazaji wa vitambulisho vya Taifa kutoka (NIDA) Makao makuu, amewataka wananchi kutambua kuwa kitambulisho cha Taifa ni nyara ya serikali hivyo kinatumiwa na mtu moja tu na ni mwiko kukitumia vinginevyo.
Amesema wananchi wenye namba za (NIDA) wanasubiri vitambulisho wanaendelea kupatiwa huduma zote muhimu sawa na walio na vitambulisho, hivyo hawapaswi kuwa na wasiwasi.
Akizungumza kwa niaba ya menejimenti ya Shirika la Posta, Afisa kutoka Shirika hilo Bwn. Stephen Kibona amewaeleza wananchi kuwa Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeingia ubia na Shirika la Posta katika zoezi la usambazaji wa vitambulisho, na Kwa kupitia mfumo wa Anwani za makazi Shirika litawafikishia hadi mahali walipo.
Kwa mujibu wa Bi. Mtui, Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa hutoa vitambulisho aina tatu kwa lengo la kuwatambulisha wananchi wazawa, wageni waliopo nchini na wakimbizi wanaoishi kisheria.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.