Makamu mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Stephen Wasira amewaasa wauguzi kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanatoa huduma nzuri na kuzingatia utu ili kuhakikisha uboreshaji mkubwa wa miundombinu uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita, unaleta tija kwa wananchi.
Mhe. Wasira ameyasema hayo alipotembelea Wilaya ya Kongwa ambapo amefanya ukaguzi wa jengo la wodi ya Wazazi katika hospitali ya Wilaya, pamoja na ujenzi wa jengo jipya la Halmashauri na kupata wasaa wa kuongea na wananchi wa Wilaya ya Kongwa katika mkutano wa hadhara.
Akisoma taarifa mbele ya Makamu Mwenyekiti kabla ya kukagua wodi ya wazazi, dkt. Thomas Mchomvu ameeleza kuwa jengo linahudumia wazazi waliotoka kujifungua, ikiwemo waliotoka kufanyiwa upasuaji ambao wanakuwa wanaendelea kupatiwa huduma, na kuongeza kuwa jengo pia lina sehemu maalum kwa ajili ya watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda wao.
Aidha dtk. Mchomvu ameeleza kuwa ongezeko la upatikanaji wa bidhaa za afya hospitalini limepunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko ya ukosefu wa bidhaa za afya na kusaidia wananchi kupata huduma hizo wanapozihitaji.
Vilevile dkt. Thomas Mchomvu ameainisha kuwa toka jengo lianze kutumika mwaka 2023, idadi ya wazazi 1097 wamepata watoto katika jengo hilo na kuongeza kuwa watoto waliozaliwa kabla ya muda wao ambao wamekuwa wakipatiwa rufaa wamekuwa wakihudumiwa kweye jengo hilo.
Aidha, Mhe. Wasira wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara, amegusia baadhi ya mafanikio katika Wilaya ya Kongwa na kueleza kuwa Serikali imefanikiwa kujenga vituo vya afya 5, zahanati 12, upatikanaji wa Maji 88%, umeme katika Vijiji vyote 87 na vitongoji 175 kati ya 176 na kuongeza kuwa katika Ilani ijayo ya Chama cha Mapinduzi, kipaumbele kimewekwa katika kukuza uchumi na kubadili maisha ya watu kwa kuweka matrekta na kukodisha kwa wakulima ili kuchochea kilimo cha umwagiliaji na ujenzi wa nyumba nzuri za wananchi.
Ziara ya makamu mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mhe. Stephen Wasira katika Wilaya ya Kongwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi kutembelea Halmashauri na Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma kujionea mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita na kupima utakelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika vipaumbele mbalimbali vinavyolenga kuwaletea wananchi maendeleo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.